Hili limekuwa kama ni fumbo gumu kwa baadhi ya wanaume.Leo nimeonelea kuileta hii mada kwenu wapenzi wa hii blog ni vitu vipi vinavyomvutia zaidi mwanamke hasa kwa mwanaume.Mwanamke atavutiwa kwako endapo utamfanyia yafuatayo:
Wanaume wengi hupuuzia hili, huona kama ni jambo lisilo na
maana sana kwao na wenzi wao. Hali ni tofauti sana kwa wanawake ambao hupenda
kuwasifia wanaume zao. Nitakupa mifano miwili ya namna wanandoa wa jinsia mbili
tofauti wanavyotambulishana kwa jamaa zao.
MWANAUME: “Peter kutana na mke wangu, anaitwa mama Diana.
Nipo naye mwaka wa tatu sasa, tuna watoto wawili, huyo Diana na mwingine
anaitwa Cris. Mama Diana, huyu ni Peter nilisoma naye A – Level, Tosamaganga
Sekondari.”
MWANAMKE: “Suzan, huyu ndiye mume wangu mpenzi...anaitwa
Elifaraja lakini mimi napenda zaidi kumuita Elly. Kiukweli nampenda sana mume
wangu jamani, tuna mtoto wetu mmoja, anaitwa Agness. (Akimgeukia mumewe) Baby,
huyu hapa ni rafiki yangu Suzan. Yaani tumekua naye mtaa mmoja huko Arusha.”
ANGALIA TOFAUTI
Bila shaka kwa namna wawili hao walivyotambulishana unaweza
kuona tofauti kubwa. Mwanaume amemtambulisha mkewe kawaida kabisa, hajaonesha
manjonjo au namna anavyompenda na kumthamini mwenzake, lakini mwanamke amefanya
hivyo.
Sikia nikuambie, KUMSIFIA mwanamke, kuna nafasi kubwa sana
kwake. Chunguza kwa makini, hata kunapokuwa na mgongano katika familia, halafu
wakatokea wageni, baada ya utambulisho na mazungumzo ya hapa na pale, wageni
wakiondoka kunakuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kumaliza mpasuko katika
familia.
Jenga utamaduni wa kumsifia mpenzi wako, unamuweka katika
kilele cha upendo. Anajiona kamili, peke yake na mwenye nguvu kwako. Anajiamini
na unamfanya azidi kukupenda kwa kuwa anaamini yupo na mwanaume ambaye
anajivunia kuwa naye.
MALENGO
Wanaume wengi wana ulemavu mmoja; hawapendi kuwashirikisha
wanawake katika mambo yao. Wanapenda kufanya mambo yao kwa siri na wakati
mwingine ikilazimika kumwambia mkewe basi kwa mshtukizo baada ya kukamilisha
jambo husika.
Hii si sahihi. Dunia ya leo imebadilika rafiki zangu.
Inawezekana wazee wa zamani walikuwa sahihi, maana ilikuwa ni suala la kununua
ng’ombe na kuwaweka katika zizi kwenye kijiji cha jirani, halafu wanapewa
malisho mazuri, baada ya miaka miwili wanazaliana, hapo ndipo anamweleza mkewe.
Siku hizi dunia imebadilika, kuna mambo mengi. Kuna suala la
hasara katika biashara, utapeli n.k. Mkeo ndiye rafiki yako mkubwa kuliko wote,
ndiye ndugu yako wa karibu zaidi kuliko yeyote. Yes! Mkeo ndiye ndugu yako
maana umetengeneza naye familia. Mmeshirikiana kuzaa watoto na kujenga maisha
pamoja.
Yeye anapaswa kujua mambo yako, ndiye mtetezi wako nambari
wani. Mweleze juu ya malengo yako, wakati mwingine anaweza kukusaidia sehemu
ambayo hukutarajia.
Hata hivyo, kumshirikisha katika malengo yako, kunampa nguvu
na nafasi ya kujiona mama katika familia yenu. Msaidizi kamili wa nyumba yenu.
KIPAUMBELE
Kuna wakati wanawake huwa na mambo yao binafsi. Kazini au
kifamilia. Inawezekana akatatizika katika eneo fulani ambalo kwa namna moja ama
nyingine atahitaji usaidizi wako. Ikitokea mkeo akawa katika hali hiyo,
msikilize.
Mathalani ana tatizo la kifamilia, amekuambia mmoja wa
wazazi wake anaumwa, msaidie. Si lazima kifedha, lakini kuonesha kujali kwako
tu, kutampa matumani kwamba anaishi na mtu sahihi. Acha kupuuza mambo yake;
hata yale madogo, kama ya ‘mtoto wa dada amerudishwa ada shuleni’.
Msikilize, mshauri panapofaa kufanya hivyo na ukiweza
msaidie hata kifedha. Katika upande wa pili ni hivyo hivyo. Labda una tatizo
binafsi, kazini kwako au kifamilia, mshirikishe.
Unaweza kushangaa jambo ambalo uliamini unaweza kulimaliza
peke yako, kwa kumshirikisha likawa
jepesi zaidi na mambo yakaendelea vyema. Kipaumbele kwa namna yoyote ile,
kunaongeza mapenzi zaidi kwa mwanamke.
TENDO LA NDOA
Hiki ni kipengele nyeti, kinachohitaji lugha nzuri ya
kirafiki kukifafanua. Hakuna siri, tendo la ndoa ni moja ya kiwakilishi cha
ndoa. Maana hata maandiko yanasema: “Mwanamke ataacha wazazi wake na kwenda kwa
mumewe, nao watakuwa mwili mmoja.”
Kimsingi tendo la ndoa lina nafasi yake. Ni muhimu
likaheshimiwa na kutengewa muda maalum wa kufurahia. Si papara. Kwa bahati
mbaya wanaume huwa si wafuatiliaji sana wa kujua namna ya kuwafurahisha zaidi
wenzao. Wenyewe wanajiwazia wenyewe. Wanafikiria namna ya kuwakomoa wenzao.
Si sahihi. Tendo la ndoa halina maana ya kukomoana. Jenga
mazoea ya kufanya maandalizi kamili kabla ya tendo. Sikiliza hisia za mwenzako.
Ukiweza kumjulia mke wako katika eneo hili, ni wazi kwamba utazidisha upendo
wake kwako, lakini pia atakuwa katika kuta za uaminifu. Akatafute nini nje
wakati wewe ndiye mganga wake unayeweza kumtibu barabara?
Kuna kitu nimesahau kweli? Kama kipo nitafute pembeni, kwa
hapa haya yatoshe kukufanya uelewe nilichotaka kukuelekeza. Nikuache na neno
moja; uamuzi wa kuijenga ndoa yako upo mikononi mwako. Ukitaka iwe
shaghalabaghala, pia ni wewe tu! Ahsante kwa kunisoma.
0 comments:
Post a Comment