Sunday, August 17, 2014

Hoja mpya zalichanganya Bunge Maalumu

By on 12:04 AM
Mwenyekiti wa Kamati Nambari 10 wa Bunge Maalumu la Katiba, Salmin Awadh Salmin akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi

  • Ni kuhusu muundo wa taasisi muhimu, Bunge, Mahakama  na nafasi za juu za uongozi
  • Sumaye ashauri Mchakato wa Katiba usimamishwe, maridhiano yafanyike


Dodoma. Mapendekezo mapya yanayopelekwa kwenye Kamati za Bunge Maalumu kwa ajili ya kurekebisha baadhi ya Ibara za Rasimu ya Katiba, yamezua mivutano mikali kiasi cha baadhi ya sura kuwekwa kiporo au kurukwa na kamati husika.
Habari zilizolifikia gazeti hili zinasema mapendekezo hayo ni yale yanayozigusa taasisi kubwa za nchi, zikiwamo Bunge la Jamhuri ya Muungano na Mahakama, pamoja na nafasi za Makamu wa Rais.
Katika baadhi ya kamati yamepelekwa mapendekezo ambayo yanataka Bunge liwe na sehemu tatu ili kutoa fursa kwa mambo ya Tanzania Bara kujadiliwa bila wabunge kutoka Zanzibar kuwapo.
“Mapendekezo yaliyopo ni kwamba wanataka Bunge liwe na sehemu tatu ambazo ni Bunge la Muungano kwa masuala ya muungano na humohumo linakuwa na sehemu mbili ambazo ni wabunge wa Zanzibar kwa ajili ya masuala ya Wazanzibari na sehemu ya Tanganyika kwa ajili ya mambo ya bara,” kilisema chanzo chetu kutoka katika kamati moja ya Bunge hilo.
Hata hivyo, habari zinasema baadhi ya wajumbe wa kamati walikosoa pendekezo hilo kwa maelezo kwamba linashabihiana na muundo wa muungano wa serikali tatu ambao ulipendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba lakini ukapingwa na baadhi ya wajumbe wakiongozwa na walio wanachama wa CCM.
Jana Mwenyekiti wa Kamati Namba 8, Job Ndugai aliwaambia waandishi wa habari kwamba kamati yake imeshindwa kuafikiana kuhusu muundo wa Bunge la Muungano hivyo kulazimika kuliacha suala hilo ili kulifanyia uchunguzi kwanza.
“Mbali na sura ya 5 inayozungumzia uraia pacha ambayo ilitusumbua, lakini pia suala la Muundo wa Bunge la Muungano na Mahakama ya Muungano vilikuwa tatizo katika kamati yangu,” alisema Ndugai.
Licha ya kwamba Ndugai hakuzungumzia suala hilo kwa undani, lakini taarifa zilizolifikia gazeti hili zinasema muundo wa kuwa na sehemu tatu katika Bunge moja ndio uliozua mtafaruku kiasi cha kamati hiyo kuliahirisha.
Katika kamati namba 5, sura ya 10 inayozungumzia suala la Bunge na Mahakama imerukwa. Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alisema: “Tumeamua kuendelea na mambo mengine kwanza maana hilo limeonekana kuwa ni gumu kwa sasa.”
Habari zaidi zinasema katika kamati hiyo namba tano, mapendekezo ya kuwapo kwa makamu wa rais watatu yalizua mjadala mkali kiasi cha kusababisha kuwapo kwa wajumbe walioamua kuandaa maoni ya wachache.
“Wamekuja na mapendekezo kwamba awepo Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye atakuwa mgombea mwenza, Makamu wa Pili wa Rais ambaye atakuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Tatu wa Rais ambaye ni Waziri Mkuu,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kamati hiyo na kuongeza:
“Lakini wapo waliokataa kama watano au sita hivi na wameamua kwamba wataandika maoni ya wachache kwa mujibu wa Kanuni ya 32 (10)”.

Saturday, August 16, 2014

Steve Nyerere kugombea ubunge jimbo la Kinondoni mwaka 2015

By on 1:07 AM

Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity, Steve Nyerere ametangaza nia yake ya kugombea ubunge mwaka 2015 katika jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa kupitia tiketi ya CCM.
Mwenekiti wa bongomovie Steve Nyerere
Mwenekiti wa bongomovie Steve Nyerere
Akizungumza na Bongo5, Steve Nyerere amesema yupo kamili na amejipanga kufanya hivyo ifikapo mwakani.
“Ukiona chereko chereko ujue mambo yameiva, yeah nitagombea ubunge mwakani. Nimejipanga na ninaweza kufanya hivyo, nipo vizuri sana,” amesema.
Katika hatua nyingine Steve Nyerere amewakaribisha watanzania wote hapo kesho katika shughuli maalum ya kuwaombea wale waliotangulia mbele ya haki itakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam kuanzia saa 4 asubuhi.

Ndege ya India iliyokuwa na abiria 280 yashuka futi 5000 angani baada ya rubani kusinzia

By on 12:59 AM

Mamlaka ya anga nchini India inachunguza tukio la hatari lililotokea Agosti 8, baada ya ndege ya Jet Airways Boeing 777-300 iliposhuka angani kwa zaidi ya futi 5000 (mita 1500) kutoka kwenye urefu waliopangiwa kuruka baada ya rubani wake kusinzia.
jet-airways
Tukio hilo lilitokea wakati ndege hiyo ikifanya safari kutoka Mumbai, India kwenda Brussels, Ubelgiji. Times of India imeripoti kuwa rubani aliyekuwa akiongoza ndege hiyo alipumzika kidogo, mapumziko ambayo kwa viwango vya kimataifa huitwa ‘controlled rest’ kwa zile ndege za masafa marefu. Safari ya ndege kutoka Mumbai hadi Brussels ni masaa 9.
Rubani msaidizi alitakiwa kuchukua majukumu yote ya kuongoza ndege kwa wakati huo, lakini inadaiwa rubani huyo wa kike alisema naye alikuwa busy na tablet ya ndege hivyo hakugundua ndege ilipoanza kushuka kutoka kwenye urefu wa futi 34,000 iliyotakiwa kuruka wakati wanapita Uturuki.
Kwa bahati nzuri waongozaji wa anga wa Uturuki waligundua kuwa ndege hiyo iliyokuwa katika anga lao imeshuka kwenye urefu (altitude) ambao umepangwa kwaajili ya ndege nyingine, na kumtaarifu rubani msaidizi arudi kwenye urefu waliopangiwa.
Marubani wote wawili wa ndege hiyo wamesimamishwa kupisha uchunguzi .
Source: Aljazeera

NDANI YA HABARI: Watoto 11 chumba kimoja, watumikishwa kuuza vitumbua

By on 12:07 AM
“Hao watoto hatujawaiba, tumewatoa kwao huko mikoani na biashara wanazofanya ni hizo ndogondogo wala siyo ngumu. Wengine hapa hawana baba wala mama wanazunguka tu mitaani. Wameona kuliko kuiba, ni bora waje wafanye kazi ili wapate pesa za kujikimu,” anasema Fatuma. 
Na Elias Msuya, Mwananchi

  • Mmiliki wa biashara hiyo asema alifanya hivyo kuwasaidia kwa kuwa wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha.


Pengine takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) kwamba watoto wapatao milioni 250 wanatumikishwa katika ajira mbalimbali duniani kote, zikawa ndogo kulingana na hali halisi kwa kuwa kila kukicha, mapya huibuka.
Ajira hizi zinapaswa kupigwa vita kwa kuwa siyo tu zinawanyima haki za msingi watoto, bali zinachochea umaskini kwa familia na taifa kwa jumla.
Hassan Abdallah mkazi wa Tabata ni mmoja kati ya wanaoshiriki katika biashara hii haramu ya kuajiri watoto. Hivi sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kuajiri watoto 11 kwa kazi za kuuza vitumbua huku akiwahifadhi ndani ya chumba kimoja.
Kati ya waajiriwa hao, watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wako wanane.
Katika makazi hayo, watoto walimwonyesha mwandishi wa habari hizi banda la mabati wanalotumia kwa malazi likiwa kando ya nyumba ya mwajiri wao.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kisukuru, Lukresia Msuya anasema kuwa Abdallah na mkewe Fatuma Shomari wamekuwa wakiwafuata watoto hao mikoani na kuwaleta jijini Dar es Salaam kuwatumikisha kuuza vitumbua mitaani.
“Tulipigiwa simu juzi na katibu wa CCM wa mtaa akisema kuwa kuna jambo la muhimu. Hapo ndipo aliponionyesha nyumba hii ambayo ina watoto wanaotumikishwa kuuza vitumbua. Tukawakusanya na kuwapelekapolisi,” anasema Msuya.
Amewataja watoto wanaoishi kwenye nyumba hiyo kuwa ni pamoja na Furaha Samuel, Steven Tudius, Amani Adison, Yusuf Simon, Richard Zakaria, Kackson Jackson Michael, Elia Wilson, Boniface Lawrence, Baraka Francis, Zamda Yumpunju, Jema Ramadhani na Haji Ramadhani.
Msuya amesema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, walikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Kisukuru kisha kuhamishia shauri hilo Stakishari ambako Abdallah aliwekwa ndani.
“Nikiwa kama mzazi inaniuma kuona watoto hawa wadogo wenye umri kati ya 17 na 12 wakifanyishwa kazi kama hizi. Nawaomba wazazi wawakumbatie watoto kama vifaranga vya kuku. Mtoto wa miaka 12 umfanyishe kazi, halafu utamlipa nini kama siyo kumdhulumu?” alihoji.
Jinsi walivyokamatwa
Akieleza jinsi alivyogundua suala hilo, katibu wa CCM wa Mtaa wa Kisukuru, Thomas Matiku anasema kuwa alipewa taarifa na wananchi wakati akitoka Buguruni.

Friday, August 15, 2014

RAIS KIKWETE AWAAPISHA MAJAJI WAPYA 20 WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA IKULU JIJINI DAR

By on 11:41 PM

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe Omar Othman Makungu pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wapya.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Rais Dkt Mohamed Gharib Bilali, Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda, Waziri wa Sheria na Katiba Dkt Asha-Rose Migiro, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema, Mtendaji Mkuu wa Mahakama Mhe Hussein kattanga katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama kuu ya Tanzania baada ya kuapishwa leo Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe Omar Othman Makungu pamoja na Majaji wa Mahakama ya Kuu Tanzania na Majaji wapya.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe Omar Othman Makungu pamoja na majaji wapya.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe Omar Othman Makungu na Jaji Kiongozi Shaban Ally Lila wakiwa katika pic ha ya jumla na Majaji wapya na wa zamani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete asubuhi ya leo, Ijumaa, Agosti 15, 2014, amewaapisha Majaji 20 wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao aliwateua mwanzoni mwa wiki hii katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam.
Halfa hiyo iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam ilihudhuriwa pia na Makamu wa Rais Mheshimiwa Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda, Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Asha Rose Migiro na Jaji Mkuu wa
Zanzibar Mheshimiwa Omar Othman Makungu.
Majaji hao wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania ni pamoja na akinamana wanane na uteuzi
huo wa Mheshimiwa Rais Kikwete umeshirikisha wanasheria kutoka Serikalini, Taasisi za Umma, Jumuia ya Afrika Mashariki, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia.
Majaji hao wapya ambao wameapishwa leo ni Jaji Penterine Muliisa Kente, Jaji Benedict Batholomew Mwingwa, Jaji Eliezer Mbuki Feleshi, Jaji John Eudes Ruhangisa, Jaji Winfrida Beatrice Korosso, Jaji Lilian Leonard Mashaka, Jaji David Eliad Mrango, Jaji Edson James Mkasimongwa, Jaji Mohamed Rashid Gwae na Jaji Firmin Nyanda Matogoro.
Wengine ni Jaji Leila Edith Mgonya, Jaji Barke Mbaraka Abdou Sehel, Jaji Awadhi Mohamed, Jaji Lugano J. Mwandambo, Jaji Rose Ally Ibrahim, Jaji Paul Kihwelu, Jaji Modesta Opiyo Makopolo, Jaji Amour Said Khamisi, Jaji Mary Caroline Levira na Jaji Salma Maghimbi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
15 Agosti, 2014

MATUKIO KATIKA PICHA: KIBANO! TRAFIKI WAMGUNGIA KZI DEREVA JEURI

By on 10:24 PM

Stori: Deogratius Mongela na gabriel ng’osha
DEREVA wa Basi la Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA) ambaye hakuweza kufahamika jina lake mara moja, amejikuta akipewa kibano hevi na askari wa usalama barabarani ‘trafiki’ baada ya kuleta ubabe wakati alipotakiwa kutii sheria bila shuruti.
Askari wa usalama barabarani ‘trafiki’ wakimdhibiti dereva wa basi la Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA) aliyevunja sheria ya usalama barabarani.
Tukio hilo la aina yake lililosababisha usumbufu kwa abiria wa basi hilo, lilitokea juzi Bamaga-Mwenge jijini Dar kufuatia dereva huyo kukataa kuegesha pembeni basi hilo lenye namba za usajili T 619 CVP lililokuwa limevunja sheria ya usalama barabarani.
Dereva huyo akionyesha ubishi wa kutotii maagizo ya 'trafiki'.
Imedaiwa kuwa, basi hilo lilishusha abiria kinyume na sheria kwenye kituo kisicho rasmi maeneo ya Chuo cha Ustawi wa Jamii, Kijitonyama, Barabara ya Shekilango.
Chanzo makini kilichoshuhudia tukio hilo kimedai kuwa, kufuatia hali hiyo ndipo trafiki hao watatu walio makini na kazi yao, walilisimamisha basi hilo ili kumsomea mashitaka dereva huyo sambamba na kondakta wake lakini wakaleta ubishi na kutoa lugha chafu kitendo ambacho trafiki hao walishindwa kukivumilia.
Askari wa usalama barabarani ‘trafiki’ wakimtoa nje dereva jeuri wa UDA.
“Waliendelea kutoa lugha chafu, hawakuonesha kutii amri ili waambiwe walichokosea ndipo trafiki wakalazimika kuwadhibiti kwa kuwafunga pingu baada ya kukataa kutii sheria bila shuruti, tunawapongeza trafiki hawa kwa kuwataiti,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya trafiki kuwadhibiti wawili hao,  mmoja wao alishika usukani, wenzake wakakaa kwenye viti na kuliendesha basi hilo hadi  Kituo cha Polisi Kijitonyama ‘Mabatini’ kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Wananchi wakishuhudia mkasa huo.
Siku za hivi karibuni kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kwamba, madereva wa mabasi ya Uda wamekuwa wakivunja sana sheria kama wao wako juu ya sheria kuliko madereva wengine.
Tunashauri madereva kuwa makini na watiifu pindi wanapokuwa barabarani ili kupunguza ajali ambazo nyingi kati ya hizo zimekuwa zikitokana na uzembe wa madereva kwa kutotii sheria za usalama barabarani-Mhariri.
JIUNGE NA GURUDUMU KWA KULIKE PAGE

HABARI PICHA:AFANDE SELE AZIMIA AKIMZIKA MKEWE!

By on 10:22 PM

Stori: Dustan Shekidele,Morogoro
Mfalme wa Rhymes Bongo, Seleman Msindi ‘Afande Sele’ ameshindwa kustahimili msiba wa mkewe, Asha Msindi (34) na kujikuta akizimia msibani wakati wa maziko, Risasi Jumamosi lina stori ya kusikitisha.
Mwili wa marehemu Asha Mohamed Shiengo 'Mama Tunda' ukiombewa kabla ya mazishi.
Tukio hilo ambalo liliibua simanzi nzito mkoani hapa na kuweka historia lilijiri juzi, Alhamisi katika Mtaa wa Amani, Mji Mkuu, alipokuwa akiishi Asha na mama yake.
Aliyekuwa mke wa Afande Sele, Asha Msindienzi za uhai wake.
RAFIKI AFUNGUKA
Kwa mujibu wa mtu wa karibu wa Afande, gwiji huyo wa muziki ambaye alitengana na mkewe mapema mwaka huu, alipopewa taarifa hizo za msiba, hakuamini hadi alipofika nyumbani kwa marehemu na kukuta watu wamejaa msibani.
Mfalme wa Rhymes Bongo, Seleman Msindi ‘Afande Sele’ akiwa amezimia msibani.
“Alipigiwa simu na baadhi ya ndugu wa mke kumueleza habari za msiba, hakushtuka sana maana hakuwa ameamini moja kwa moja hivyo akasema ataamini atakapofika msibani na kukuta msiba,” alisema mtu huyo wa karibu ambaye aliomba hifadhi ya jina gazeti.
Afande Sele akiweka udongo kwenye kaburi la mke wake Mama Tunda.
AZIMIA
Mtu huyo wa karibu alizidi kueleza kuwa, mara baada ya kufika nyumbani hapo na kukuta ndugu, jamaa na marafiki wamekusanyika ndipo Afande alipoanguka na kuzimia kwa takriban saa nne kisha akaziduka.
“Alipofika pale nyumbani kwa mkewe na kukuta umati ukiwa msibani, alijitahidi akaingia ndani na alipomuona mama mkwe wake, hapohapo alianguka na  kuzimia,” alisema mtu huyo.
Mama wa marehemu Asha Msindi (34), Hamida Rajab Sulu.
APEPEWA
Rafiki huyo wa Afande alizidi kueleza kwamba, baada ya kuzimia, ndugu wa mke walimlaza kwenye kochi kisha baadaye rafiki zake walimchukua na kumpeleka nyumbani kwake maeneo ya Msufini ambapo walimpepea kisha wakammwagia maji ya baridi, akazinduka.
Alipozinduka, aliwaomba marafiki zake wampeleke tena msibani ambapo alipofika aliomba kuletewa mwanaye mdogo, Asantesanaa, akambeba na kukaa naye msibani hapo.
Majirani waliofika msibani wakiwa pamoja na mama wa marehemu(Asha Msindi), Hamida Rajab Sulu(wa kwanza kulia).
CHANZO CHA KIFO
Akizungumza na mwandishi wetu, mama mzazi wa marehemu, Hamida Rajab Sulu, alisema kuwa mwanaye alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa malaria kali kwa takriban siku tatu, ndipo Jumatano iliyopita asubuhi walipompeleka katika Hospitali ya St. Mary mjini hapa.
Alisema kuwa alipofikishwa hospitalini hapa alilazwa na kuanzishiwa dozi ya malaria lakini baadaye hali ilizidi kuwa mbaya wakalazimika kumuhamishia kwenye Hospitali ya Manispaa ya Morogoro.
“Walimlaza pale kwa saa kadhaa, walipoona hali inazidi kuwa mbaya, walitushauri tumuhamishie kwenye Hospitali ya Manispaa Morogoro.“Tulipofika pale walimuanzishia dripu ya kutibu malaria, kabla hata haijaisha, mgonjwa alianza kutikisa miguu, hapohapo akafariki dunia. Ilikuwa muda wa saa 5:00 usiku,” alisema mama huyo.
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania 'TAFF', Simon Mwakifwamba akimpa pole Afande Sele.
WASANII WATINGA MSIBANI
Msiba huo umeacha historia ya aina yake kwani kesho yake asubuhi (Alhamisi), wasanii wengi walifika msibani hapo kwa ajili ya kuomboleza hali ambayo iliwafanya baadhi ya watu kushangaa wasanii badala ya kuomboleza.
Picha ya familia: Kutoka kulia ni Asha Mohammed Shiengo ‘Mama Tunda’ enzi za uhai wake, Selemani Msindi ‘Afande Sele’, Asantesana Selemani na Tunda Selemani.
Miongoni mwa wasanii ambao walifika mapema msibani hapo ni pamoja na Rais wa Shirikisho la Filamu Nchini, Simon Mwakifwamba na Joseph Haule ‘Profesa Jay’.
AFANDE ANENA
Akizungumza kwa uchungu makaburini hapo, Afande Sele alisema kifo cha mkewe ni pigo kubwa maishani mwake kwani ndiye aliyekuwa faraja ya pekee kwa wanaye, Tunda na Asantesanaa.
“Hili ni pigo kubwa maishani mwangu, mama Tunda alikuwa ndiye kila kitu kwa wanangu, inaniuma sana,” alisema Afande akitokwa machozi.
Mwanamuziki Profesa Jay (kulia) akimfariji Afande Sele.
AZIKWA
Baada ya umati kujikusanya msibani hapo, taratibu za mazishi zilifanyika siku hiyohiyo na wakaelekea kuzika kwenye Makaburi ya Kola mjini hapa.
TUJIKUMBUSHE
Kabla Afande Sele na mama Tunda hawajatengana mapema mwaka huu, waliishi kama mume na mke kwa zaidi ya miaka kumi na kufanikiwa kupata watoto wawili, Tunda na Asantesanaa.