Na Waandishi Wetu, Mwananchi
- Ni kuhusu muundo wa taasisi muhimu, Bunge, Mahakama na nafasi za juu za uongozi
- Sumaye ashauri Mchakato wa Katiba usimamishwe, maridhiano yafanyike
Dodoma. Mapendekezo mapya
yanayopelekwa kwenye Kamati za Bunge Maalumu kwa ajili ya kurekebisha
baadhi ya Ibara za Rasimu ya Katiba, yamezua mivutano mikali kiasi cha
baadhi ya sura kuwekwa kiporo au kurukwa na kamati husika.
Habari zilizolifikia gazeti hili zinasema
mapendekezo hayo ni yale yanayozigusa taasisi kubwa za nchi, zikiwamo
Bunge la Jamhuri ya Muungano na Mahakama, pamoja na nafasi za Makamu wa
Rais.
Katika baadhi ya kamati yamepelekwa mapendekezo
ambayo yanataka Bunge liwe na sehemu tatu ili kutoa fursa kwa mambo ya
Tanzania Bara kujadiliwa bila wabunge kutoka Zanzibar kuwapo.
“Mapendekezo yaliyopo ni kwamba wanataka Bunge
liwe na sehemu tatu ambazo ni Bunge la Muungano kwa masuala ya muungano
na humohumo linakuwa na sehemu mbili ambazo ni wabunge wa Zanzibar kwa
ajili ya masuala ya Wazanzibari na sehemu ya Tanganyika kwa ajili ya
mambo ya bara,” kilisema chanzo chetu kutoka katika kamati moja ya Bunge
hilo.
Hata hivyo, habari zinasema baadhi ya wajumbe wa
kamati walikosoa pendekezo hilo kwa maelezo kwamba linashabihiana na
muundo wa muungano wa serikali tatu ambao ulipendekezwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba lakini ukapingwa na baadhi ya wajumbe wakiongozwa
na walio wanachama wa CCM.
Jana Mwenyekiti wa Kamati Namba 8, Job Ndugai
aliwaambia waandishi wa habari kwamba kamati yake imeshindwa kuafikiana
kuhusu muundo wa Bunge la Muungano hivyo kulazimika kuliacha suala hilo
ili kulifanyia uchunguzi kwanza.
“Mbali na sura ya 5 inayozungumzia uraia pacha
ambayo ilitusumbua, lakini pia suala la Muundo wa Bunge la Muungano na
Mahakama ya Muungano vilikuwa tatizo katika kamati yangu,” alisema
Ndugai.
Licha ya kwamba Ndugai hakuzungumzia suala hilo
kwa undani, lakini taarifa zilizolifikia gazeti hili zinasema muundo wa
kuwa na sehemu tatu katika Bunge moja ndio uliozua mtafaruku kiasi cha
kamati hiyo kuliahirisha.
Katika kamati namba 5, sura ya 10 inayozungumzia
suala la Bunge na Mahakama imerukwa. Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo
alisema: “Tumeamua kuendelea na mambo mengine kwanza maana hilo
limeonekana kuwa ni gumu kwa sasa.”
Habari zaidi zinasema katika kamati hiyo namba
tano, mapendekezo ya kuwapo kwa makamu wa rais watatu yalizua mjadala
mkali kiasi cha kusababisha kuwapo kwa wajumbe walioamua kuandaa maoni
ya wachache.
“Wamekuja na mapendekezo kwamba awepo Makamu wa
Kwanza wa Rais ambaye atakuwa mgombea mwenza, Makamu wa Pili wa Rais
ambaye atakuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Tatu wa Rais ambaye ni
Waziri Mkuu,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kamati hiyo na
kuongeza:
“Lakini wapo waliokataa kama watano au sita hivi
na wameamua kwamba wataandika maoni ya wachache kwa mujibu wa Kanuni ya
32 (10)”.
0 comments:
Post a Comment