Sunday, August 17, 2014

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Awataka UKAWA Warudi Bungeni…Asisitiza kuwa Rais Kikwete hana Mamlaka kisheria ya Kulivunja Bunge hilo

By on 9:45 PM

Mwanasheria mkuu wa serikali nchini Tanzania Jaji Fredrick Werema amesema hakuna sheria inayompa mamlaka Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kulivunja bunge maalum la katiba hivyo amewataka umoja wa katiba ya wananchi UKAWA kurejea katika bunge hilo kwa lengo la kupata maridhiano ya pamoja.
Jaji Werema amesema hayo jana jijini Dar es salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kufafanua masuala kadhaa yanayohusiana na mwenendo mzima wa Bunge Maalum la Katiba na madai ya umoja wa katiba ya wananchi UKAWA.
Akitumia muda mwingi kufafanua baadhi ya vifungu katika sheria ya mabadiliko ya Katiba, Jaji Werema amesema siyo kweli kwamba Bunge hilo halina mamlaka ya kubadilisha vifungu vya Rasimu, na kusema kuwa kama ingekuwa hivyo, basi kusingekuwa na haja ya kuwepo kwa Bunge hilo.
Kwa kutumia kifungu cha 25 cha Sheria hiyo, Jaji Werema amesema kuwa Bunge hilo limepewa kazi ya kupokea Rasimu, kuijadili, kuiboresha, na kutoa Katiba inayopendekezwa.
Amesema baada ya hapo, litatunga na kupitisha masharti ya mpito na masharti yatokanayo bila kuingiliwa na mtu, kabla ya ukomo wake.
Kuhusiana na madai ya kwamba Rais anaweza kulivunja Bunge hilo, Jaji Werema amesema kuwa Rais hana mamlaka hayo kabla bunge hilo halijamaliza kazi yake na kwamba hakuna mtu yeyote mwenye uwezo huo kwa mujibu wa sheria.
“Hakuna Ugunduzi mzuri uliowahi kufanywa na mwanadamu kama ugunduzi wa Sheria na utawala wa Sheria, hayo ni maandishi tu lakini lazima kila mtu ayafuate” Alisema Werema na kuongeza kuwa..
MWANASHERIA
“Ninamuambia Rais kuwa Rais huna mamlaka ya kusimamisha Bunge la Katiba kwa mujibu wa sheria”
Werema ameongeza kwamba kama lengo la kusitisha vikao vya bunge kwa ajili ya maridhiano, hakuna haja ya kufanya hivyo ka kuwa pande mbili zinazolumbana, kila upande unang’ang’ania maslahi yake, hali inayopelekea kusiwe na dalili za usuluhishi.
SHERIA
Kutokana na hilo, amesema kuwa msuluhishi pekee atakuwa ni mwananchi wakati wa kupiga kura ya maoni na kwamba hivi sasa mjadala wa sura ya Kwanza na Sita umekwisha fungwa.
Werema pia amekiri kuwepo na baadhi ya watu ndani ya CCM wenye mtazamo tofauti lakini hawajasusia Bunge, na kwa kuwa wanafuata misingi ya demokrasia, wakishindwa hoja zao, hukubaliana na hoja zinazoungwa mkono na wengi.

0 comments:

Post a Comment