Rais
Jakaya Kikwete amesema dhamira ya Serikali ni kuinua maisha ya
Watanzania na dhamira hiyo iko pale pale na kwamba wanaofikiri nia hiyo
ni kuwajaza wao fedha mifukoni uwezo huo haupo.
Rais
alitoa kauli hiyo jana katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakati
akizindua ujenzi wa barabara ya Mbande hadi Kongwa, itakayojengwa kwa
kiwango cha lami.
Alisema dhamira ya Serikali ya kuinua maisha ya Watanzania haina maana kuwa wananchi watapewa fedha za kuweka mifukoni mwao.
Alisema
dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo itafikiwa kwa kupitia
uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, shule, njia za
mawasiliano ili kurahisisha kuweza kufikia malengo yao.
“Wengine tunaposema kuinua maisha ya Watanzania wanafikiri ni kumwaga fedha mifukoni mwao uwezo haupo,” alisema.
Pia
alisema Serikali imeboresha ukusanyaji wa fedha za ndani ili kuongeza
mapato na kuondoa utegemezi katika miradi ya maendeleo.
Rais
Kikwete alisema makusanyo ya mapato yameongeka kutoka bilioni 170 kwa
mwezi hadi bilioni 900 kwa mwezi hivi sasa na ongezeko la fedha hizo
linasaidia ujenzi wa barabara za viwango vya lami na hata zile za
vijijini.
Aidha alisema Serikali inafikiria kuongeza barabara za lami mbili au tatu za ndani katika wilaya hiyo ya Kongwa.
“Tumetimiza ahadi kwenye maeneo mengi na tunaahidi kuendeleza uwekezaji kwenye barabara, umeme na maji,” alisema.
Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli alisema mradi wa barabara kutoka Mbande hadi Kongwa ni moja ya ahadi katika ilani ya CCM.
Alisema
sehemu ya ujenzi wa barabara hiyo iliyozinduliwa ni kielelezo tosha
kuwa serikali imedhamiria kujenga barabara kwa ajili ya kuwaletea
wananchi wake maendeleo.
“Barabara
hii imezinduliwa na Rais ambaye anatoka CCM na mnatakiwa kuhakikisha
Rais ajaye anatoka CCM ili aendeleze kazi iliyoanzishwa, haiwezekani
barabara hii ije kufunguliwa na Rais wa kutoka chama kingine,” alisema.
Alisema barabara nyingi zinajengwa kwa kutumia fedha za ndani kwa asilimia 100 bila kutegemea wafadhili.
“Tanzania ni moja ya nchi zinazojengwa barabara zenye viwango vya ndani kwa kutumia fedha zake za ndani,” alisema.
Alisema Serikali itatoa bilioni moja kwa ajli ya kusaidia ujenzi wa barabara za vijijini katika Wilaya ya Kongwa.
Kwa
upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads)
Mhandisi Patrick Mfugale alisema barabara iliyozinduliwa ni sehemu ya
barabara yenye urefu wa kilometa 101.7 ya kutoka Mbande hadi Kibakwe.
Alisema ujenzi wa barabara iliyozinduliwa yenye urefu wa kilometa tano asilimia 85 ya kazi yote imekamilika.
0 comments:
Post a Comment