Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe jana
alikabidhiwa fomu na makada wa chama hicho na kumtaka awanie tena kiti
hicho, ombi ambalo alilikubali na kufungua milango kwa wanachama wengine
‘kupimana naye kifua’.
“Nafasi bado ipo, anayetaka kupima kifua na mimi ajitokeze. Tena nawaomba viongozi wangu msizuie fomu kwa anayetaka,” alisema Mbowe ambaye ameongoza chama hicho kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.
Makada
wa chama hicho kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiongozwa na kada
maarufu, Athuman Mzigo (Mapigo Saba) kutoka Kigoma, walikutana na Mbowe
na kuwasilisha maombi yao ya kumtaka awanie tena nafasi hiyo.
“Kutokana na sifa za mwenyekiti wetu, tumechangishana Sh200 kila mmoja hadi zikafika Sh50,000,” alisema Mapigo Saba huku akishangiliwa na makada wenzake alioambatana nao na kuongeza:
“Tumemwomba
mwenyekiti agombee nafasi hiyo kwa kuzingatia sifa; kwanza anaijua
vizuri idadi ya Watanzania na matatizo yao, pili anaungwa mkono na watu
wengi na amekisaidia chama kukua. Tulikuwa na madiwani 40 leo wamefika
500, wabunge watano leo 48. Halafu hana ubaguzi ndiyo maana ameunganisha
vyama vya upinzani na kuunda Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi).”
Huku
akichomekea maneno ya lugha ya Kiha, Mapigo Saba alisema kuwa maombi ya
kumtaka Mbowe agombee pia yametolewa katika mikoa ya Rukwa, Manyara,
Iringa, Njombe, Jimbo la Same Magharibi, Zanzibar, Mwanza na
Kilimanjaro.
Hotuba
ya Mapigo Saba ilifuatiwa na salamu kutoka kwa wazee wa wilaya za
Kinondoni, Ilala na Temeke, Baraza la Wanawake (Bawacha) na Baraza la
Vijana (Bavicha).
Akitoa
salamu za Bavicha, mwenyekiti wa baraza hilo Njombe, Emmanuel Masonga
alisema Mbowe ni sawa na Joshua aliyemalizia kuwaongoza wana wa Israel
kuingia nchi ya Kanaani:
“Sisi
Wakristo tunajua kuwa Mussa alianzisha safari ya Waisrael kwenda
Kanaani, ila hakuwafikisha. Kina Mtei (Edwin), Kimesera (Victor), Bob
Makani na wengineo walianzisha safari ya kwenda Ikulu, ila
hawakutufikisha. Mbowe ni sawa na Joshua atakayetufikisha Ikulu,” alisema Masonga.
Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Susan Lymo alimsifu Mbowe akisema ameongeza hamasa ya wanawake kushiriki siasa katika chama hicho.
“Mwaka
2000, kulikuwa na mwanamke mmoja katika viti maalumu, mwaka 2005
waliongezeka na kufikia sita na mwaka 2010 wamefikia 26. Mwenyekiti pia
ameufanya mwaka huu kuwa wa wanawake kitaifa na ameongeza hamasa ya
wanawake kushiriki siasa,” alisema Lymo.
Mbali
na viongozi wa chama, alikuwapo pia Sheikh Rajab Katimba kutoka Jumuiya
na Taasisi za Kiislamu ambaye alimsifu Mbowe na kuomba agombee tena
nafasi hiyo.
Mbowe akubali
Baada
ya Mratibu wa Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Nickson Tugara kummwagia
sifa Mbowe, Mapigo Saba alimkabidhi fomu, huku makada wakiimba, ‘Jembe,
jembe, jembe…”Mbowe aliishukuru Kamati Kuu ya chama hicho kwa kupanga uchaguzi Septemba 14, mwaka huu ambayo ni siku yake ya kuzaliwa huku akiahidi kujenga chama imara.
“Mtaiona Chadema mpya ifikapo Septemba 14. Hiki chama hakitakufa na hatutamvumilia mtu yeyote wa kabila lolote atakayekivuruga,” alisema.
Mbowe alisema hajawahi kuomba kugombea uenyekiti wa chama hicho tangu aliponza mwaka 2000…
“Napata wakati mgumu ninapofikia wakati huu. Chadema ina watu mbalimbali wenye taaluma na uzoefu, kwa nini mimi? Makundi haya yaliyojitokeza kunichukulia fomu yanaweza kutafsiriwa na wapenda majungu kuwa nimepanga mimi.
“Leo ni mara ya tatu naombwa kugombea uenyekiti, sijawahi kuomba. Mwaka 2004, Mzee Makani aliniomba nikamkatalia, lakini akaunda kikundi cha wazee walionichukulia fomu.
“Mwaka 2005, chama hakikuwa na mgombea urais, awali alijitokeza Profesa Mwesiga Baregu lakini akajitoa, nikaambiwa nibebe mzigo. Mwaka 2009 nikaombwa tena kugombea.”
Alisema amedhamiria kujenga chama kimtandao na kimfumo ili kuondokana na mfumo wa kienyeji… “Huko nyuma wakati wa uchaguzi watu walipeana tu nyadhifa kiundugu tukadhani chama kimeongezeka. Lakini wakati huu uchaguzi umefanyika kwa miezi tisa.
“Tulisema hatuwezi kufanya uchaguzi wa Taifa bila kupata viongozi wa mkoa, wilaya, kata, kijiji na mtaa, kitongoji na shina.
Tumefanya
uchaguzi, watu wamepima na kuona mambo magumu, mara unasikia wanakimbia
wakisema wameacha uenyekiti, uache wakati chama kinakua?”
0 comments:
Post a Comment