Vilio
na simanzi jana vilitawala kwa wakazi wa maeneo ya Sinai-Mabatini,
baada ya vifo vya watu wanne wa familia mbili tofauti, vilivyotokana na
mvua iliyosababisha miamba mikubwa ya mawe kuporomoka na kuponda nyumba
zao usiku wa manane.
Tukio
hilo la kusikitisha limeripotiwa kutokea saa nane usiku kuamkia jana,
wakati mvua iliyoambatana na upepo wa wastani ilipokuwa ikiendelea
kunyesha, na kusababisha miamba hiyo mikubwa inayokadiriwa kufikia tani
mbili kuporomoka na kuziponda nyumba hizo na kusababisha vifo hivyo na
majeruhi wanne.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari wakati wa mvua.
Mpekuzi
ilifanikiwa kufika eneo la tukio na kushuhudia miamba hiyo ikiwa
imeharibu nyumba, huku nyumba moja iliyojengwa kwa matofali ya tope
ikiwa imeanguka na kubaki kifusi.
Nyumba
zilizokumbwa na maafa hayo zinamilikiwa na watu waliotajwa kwa majina
ya Joseph William na Lameck Ajiji, na kila moja watu wawili wamefariki
kwa kukandamizwa na miamba hiyo.
Katika
nyumba ya William iliyokuwa na watu watano, waliofariki wametajwa kuwa
ni Kefa Joseph (15) na Emmanuel Joseph (12), wote wanafunzi wa Shule ya
Msingi Mbugani na majeruhi mmoja ambaye hakufahamika jina lake ambaye
alikimbizwa hospitali.
Nyumba
inayomilikiwa na Ajiji yenye watu watatu, waliofariki wametambuliwa
kuwa ni mama wa nyumba hiyo, Kwinta Geko (24) na mumewe Samson Odinya.
Waliojeruhiwa ni mtoto Bety Samson (4) na Godfrey Joseph (14) mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbugani.
Tukio
hilo ni la pili kutokea katika eneo hilo la Sinai. Mara ya kwanza
ilikuwa ni mwaka 2009 baada ya miamba kuporomoka na kusababisha vifo vya
watu wawili wa familia moja.
Mamia ya wananchi waliofika eneo hilo, walijitolea kwa kumpa fedha mtoto Bety aliyenusurika kufa kutokana na tukio hilo.
Mbunge
wa Nyamagana jijini Mwanza, Ezekiel Wenje (Chadema), alifika eneo la
tukio na kutoa pole kwa wananchi, ndugu jamaa na marafiki wa familia
zilizoathirika na janga hilo, ambapo alionyesha kushtuka baada ya
kuelezwa na wananchi kwamba hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyefika
eneo hilo.
Akizungumza kwa kutumia kipaza sauti mbele ya umati wa watu waliokuwa wamefurika katika eneo hilo la tukio, alisema: “Inashangaza sana kuona hata mkuu wa wilaya hajafika hapa. Nitawasiliana na viongozi wa Serikali na mchana nitarudi hapa tena.”
Baadhi
ya wananchi waliozungumza na Mwandishi katika eneo la tukio, waliiomba
Serikali kuzuia wananchi kujenga karibu na miamba mikubwa, kwani kufanya
hivyo itasaidia sana kuepusha maafa kama hayo.
“Kwa
kweli tukio hili linasikitisha sana, na tunaomba viongozi wa serikali
wasaidie wananchi kuwaondosha kwenye maeneo ya kwenye miamba,” alisema mmoja wa wananchi hao ambaye pia ni balozi wa Shina Namba Tano, Mtaa wa Nyerere A, Jackson Kitundu.
0 comments:
Post a Comment