Wakati bado msimamo wa Wajumbe wa Bunge la Katiba wa kundi la Ukawa
ukiwa haufahamiki kama watarejea bungeni kuendelea na vikao hivyo mwezi
Agosti au la, mjadala wa katiba mpya umechukua sura mpya, baada ya Spika
wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, kuungana na viongozi wa
CCM kukibeza kikundi hicho.
Kwa kauli hiyo, Spika Kificho anaungana na Mawaziri wa SMZ katika
kubeza uamuzi huo wa Ukawa, ingawa yeye akaenda mbali zaidi na kumtupia
lawama Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba akieleza kuwa alimlisha maneno.
Kificho kwa mara ya kwanza amechomoza katika mkutano wa hadhara wa
CCM uliofanyika Uwanja wa Kwamabata eneo la Magogoni na kusema hakukuwa
na uamuzi wa pamoja wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kupendekeza
Serikali tatu. Akasema dai hilo lilichomekwa na Tume ya Jaji Joseph
Warioba iliyokusanya maoni ya watu kuhusu katiba.
Kificho amewaeleza wananchi kuwa yeye amezaliwa ndani ya Afro Shiraz
(ASP), akalelelewa na kukulia CCM, hivyo hathubutu, hatathubu na
hakuthubutu kusaini waraka wa kutaka mamlaka huru ya Dola ya Zanzibar
ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mara nyingine Kificho anaonekana kusafisha upepo mchafu uliokuwa
ukivuma na kutaka kumpeperusha ndani ya chama chake huku baadhi ya
wanachama na viongozi wenzake, wakimtaja kama mtu aliyeshiriki kutaka
kuwasaliti na kuwazunguuka mbuyu.
Madai ya awali ya viongozi wenzake akiwemo Mnadhimu wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar upande wa CCM Salmin Awadh Salmin, yanamtupia
lawama Kificho na kumpasha hakukuwa na kikao chochote kilichoketi na
kupitisha azimio la BLW kutaka Serikali tatu au mamlaka kamili ya
Zanzibar nje Muungano uliopo.
Mvutano huo ulioibuka nje ya Bunge la Katiba, huenda ndiyo
ulioambukiza mipasho, piga nikupige ya maneno na kutupiana vijembe
vikali kati ya wabunge wa Bunge la Katiba wa CCM na CUF kabla ya kundi
la Ukawa halijaamua kuliacha bunge na kusema wamechoshwa na matusi,
kejeli na ubaguzi.
Kificho akihutubia mkutano wa hadhara, akasema amekuwa Mwakilishi wa
CCM Jimbo la Makunduchi kwa miaka saba, akawa spika miaka 19,
akijinasibu kuwa ni spika mzoefu baada ya Chifu Adam Sapi Mkwawa, kufika
kwake alipo sasa kumetokana na nguvu za CCM, hivyo hana jeuri ya
kusaliti sera za chama chake.
Akizungumza kwa kujiamni na kujiosha, akamtupia shutuma Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Warioba akisema kuwa ndiye
aliyemwandalia fitina hiyo.
Hata hivyo, waraka ulioandikwa na kusainiwa na Spika Kificho
umeandikwa na kutaja bayana kuwa Azimio la BLW Zanzibar ni kuhitaji
mamlaka huru ya Dola, jambo ambalo limechukuliwa na wengi kama
linalohitaji serikali yenye mamlaka kamili Zanzibar.
Kificho anasema kilichomo kwenye waraka huo ni hitaji la kufanyika
marekebisho na mageuzi makubwa ya msingi ili kuipa Zanzibar nyenzo za
kujijenga kiuchumi na kujitegemea ijiendeshe kwa kusimamia mambo
yasiokuwa ya Muuungano kwa uwazi na si kupigania mamlaka huru ya Dola .
Pia ameeleza kuwa katika moja ya waraka huo kulikuwa na kosa la
kitaalamu katika uandikaji na tafsri ya kila anayeusoma kutoa fasiri
aitakayo, lakini si kusudio la BLW au lake kutaka mamlaka huru ya Dola.
Imeelezwa kuwa wawakilishi watano ndiyo waliojadili na kutia saini
zao kwenye waraka huo na Kamati ya Kudumu ya Uongozi ya BLW ikakwepwa.
Wajumbe hao ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Abuboubakary
Khamis (Mgogoni) ,Spika Kificho, Hamza Hassan Juma (Kwamtipura), Katibu
wa BLW Zanzibar Yahya Khamis Hamad na Mgeni Hassan Juma (Viti Maalum).
Hata hivyo Mwakilishi Hamza Hassan Juma (Kwamtipura) Makame Mshimba
Mbarouk (Kitope )Asha Bakari Makame( Viti maalum), Mwakilishi Mohamed
Raza (Uzini), aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki (amefukuzwa CCM)
Mansour Yussuf Himid, Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee ni kati ya vigogo
wa CCM waliosimama kidete kukosoa masuala kadhaa ndani ya Muungano
kabla ya Bunge la Katiba kuanza na Ukawa kuzaliwa.
Katika semina iliyoitishwa na Baraza la Wawakilishi, wajumbe hao kwa
kiasi kikubwa walisimama na kueleza kuwa kimsingi hawakuridhika na
waraka huo.
Hayo na mengine wakati yakijiri na kupita katika siasa za Zanzibar,
Msemaji wa CUF Salum Abdallah Bimani, ameeleza kuwa haikuwa mwafaka kwa
Spika Kificho kupanda kwenye majukwaa ya kisiasa na kuzungumzia msimamo
wa BLW na kumtupia lawama Jaji Warioba.
Bimana anasema kama ataendelea kupanda majukwani na kukanusha msimamo
wa BLW, hawatasita kumrushia paka wa kisasa na kuweka kila kitu
hadharani ikiwa ni pamoja na kuanika waraka wake aliousaini kwa niaba ya
taasisi anayoiongoza.
Analitaja Baraza ni moja kati ya mihimili mitatu inayounda Serikali
hivyo hakupaswa kiongozi wa mhimili kusimama na kutoa msimamo wa
kitaasisi na kusema hatua hiyo inaweza kutafsiariwa ni ukiukaji wa
taratibu za kidsemokrasia na uvunjaji wa mipaka yake.
Hata hivyo wakati tuhuma hiyo wa Bimani ikoinekana kumponda na
kumbeza Spika Kificho kwa madai hayo ya taasisi anayoiongoza ni kinyume
na miiko ya demokrasia na mgawanyo wa madaraka, Naibnu Katibu Mkuu wa
UVCCM Zanzibar Shaka Hamdu Shaka, amemtaka Bimani kwaanza aondoe boriti
kwenye jicho lake ndipo atoa kibanzi kwenye jicho la mwenzake.
Shaka anasema ingefaa sana kama Bimani angekuwa jasiri wa
kumnyamazisha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
ambaye pia ana dhamana ya taasisi ya serikali lakini akituimia kofia ya
kisiasa kama Katibu Mkuu akizungumzia masuala ya kisiasa na kuafiki
msimamo wa Ukawa.
Vyovyote itakavyokuwa, kimsingi na kiuhalisia kuna umuhimu pande
mbili za kisiasa kati ya wabunge wa bunge la katiba chama tawala na
kundi la Ukawa kukaa kitako , kutafakari, kuafikiana na kuridhiana ili
Taifa lipate katiba mpya mwakani.
0 comments:
Post a Comment