Baada
ya watu na taasisi kadhaa kudai kitendo cha Bunge Maalumu la Katiba
kupokea maoni ya wananchi na kuyaongeza kwenye rasimu ya Katiba mpya, ni
kuingilia kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mwenyekiti wa Bunge
hilo, Samwel Sitta, alisema bunge hilo lina mamlaka makubwa kuliko tume
hiyo.
Amesema
hata wajumbe wa bunge hilo wanaoendelea kupitia rasimu hiyo, siyo
mazuzu, wana akili zao, wasomi na wapo watu wengi wanaotambua kazi hiyo
na kuipongeza.
Sitta alivunja ukimya huo na kutoa ufafanuzi jana mbele ya
waandishi
wa habari kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma, na kuongeza kuwa
wananchi wameona rasimu ya Katiba mpya, ina upungufu.
“Mimi
naelewa kuna watu wanakasirishwa sana na kazi tunayoendelea kuifanya,
ni haki yao kukasirika lakini kinachofanywa ni wananchi ambao
hatukuwaalika, wanakuja kwa makundi kuelezea wanachoona kuwa ni upungufu
ndani ya rasimu, sasa haya watayapeleka wapi?
“Hii
hali ya kuonekana sisi Bunge na Tume tupo hadhi moja si kweli, Tume ina
mamlaka yake lakini Bunge lina mamlaka makubwa zaidi ya Tume…
waliotunga sheria waliona ipo kazi inayofanyika pamoja na kufanya
marekebisho ndio maana wanachotoa wao ni rasimu sisi tutakachotoa
inaitwa Katiba inayopendekezwa.”
Alisema
dhana kwamba lolote likifanywa kwenye rasimu ni usaliti kwa nchi au
inachakachuliwa, msingi wake ni ghadhabu za mtu na uamuzi tu wa kuwaona
waliopo Dodoma ni mazuzu.
“Hapa
kuna watu wasomi wazuri tu wenye akili zao. Kusema tunafanya kazi ya
Tume ni upotoshaji mwingine wa watu wasiotakia mema Bunge Maalumu la
Katiba. Sijui kwa nini rasimu inapewa hadhi kama msahafu, wakati
imeandikwa na binadamu tu ina upungufu mkubwa.
“Mtaona kuanzia Septemba 2 mijadala ya hoja itakavyokuwa.
Wananchi
wao wameona Tume haikuwatendea haki maoni yao waliyoyatoa, na waliona
mahali pa kwenda kwenye chombo cha juu zaidi nacho ni Bunge Maalumu la
Katiba, tuna wajibu wa kuwapokea kwani tupo kwenye kazi ya kutunga
Katiba”.
Alisema
kazi inayofanyika, ni kutoa Katiba rafiki kwa wananchi na kutoa mfano
wa wasanii, ambao waliona pamoja na kutoa maoni kwa maandishi,
hayakuzingatiwa na Tume lakini Bunge kwa vigezo vyake, limeona
inastahili.
“Wamekuja
wakitaka kwenye rasimu kuwekwe kipengele cha mali isiyoshikika, yaani
haki miliki bunifu nasi tumeona inastahili, lakini Tume waliiacha nasi
tumeongezea kwenye sehemu rasimu iliyoweka mali tu,” alisema.
Miongoni
mwa vipengele vilivyoongezwa kwenye rasimu hiyo, ni masuala ya Serikali
za Mitaa, yaliyotokana na andiko la aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ambayo yalipangwa kuwepo
kwenye Katiba ya Serikali ya Tanganyika, ambayo ni ardhi, mazingira,
rasilimali za Taifa na haki za watumiaji wa bidhaa.
Kwa
upande wa Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Ummy Mwalimu, alisema Kamati
yake imeshapitisha sura zote kwa kupata theluthi mbili kila upande,
lakini suala la akaunti ya pamoja kwa Tanzania Bara na Zanzibar,
hawakufanya uamuzi.
Alisema
wajumbe wa kamati hiyo, walitaka suala hilo liwekwe kiporo hadi baada
ya kukamilika kwa semina ya wataalamu wa masuala ya fedha, waliokuwa
wakiwapa jana kuhusu mgawanyo huo wa fedha.
“Tunataka
tujue kwa sasa hali ikoje, changamoto zake na wapi kwenye kero. Kwenye
suala hili wajumbe walibishana sana na waliweka pembeni itikadi za vyama
vyao vya siasa,” alisema.
Naye
Makamu Mwenyekiti wa Kamati Namba 11, Hamad Masauni Yusuf, alisema
Kamati yake imeshapiga kura kwenye sura zote na changamoto kubwa
waliyokumbana nayo, ni suala la fedha za pamoja.
“Leo
(jana) tunategemea kupata elimu kutoka kwa wataalamu wa fedha na
tukiona kuna mambo muhimu, itatubidi tuitishe kikao cha dharura kufanya
marekebisho. Lengo ni pamoja na masuala ya fedha. Pia Muungano
uimarishwe na kusiwe na mambo ya kuutatiza na pande zote mbili
zifaidike,” alisema.
Mwenyekiti
Kamati Namba Nne, Christopher ole Sendeka, ambaye hakuwepo kwa muda
mrefu kuhudhuria kamati kutokana na kuuguliwa na watu wa familia yake,
alisema kutokuwepo kwake hakupaswi kuonekana kuwa anaunga mkono Ukawa.
Alisema kwenye kamati yake kulikuwa na mjadala mkali na watu walikuwa wakali lakini mwishowe walielewana vizuri.
Alitaja
maeneo yaliyosababisha wajumbe kuwa wakali kuwa ni ardhi, uraia pacha,
masuala ya wakulima na wafugaji na muundo wa Bunge.
Mwenyekiti
wa Kamati Namba Tatu, Dk Francis Michael, alisema kwenye Kamati yake
walipingana sana na kuvutana na kufanikiwa kupata makubaliano mazuri na
kila sura kupata theluthi mbili kwenye sura zote.