Wednesday, July 9, 2014

Taarifa zaidi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai kuhusu bomu lililolipuka Arusha

By on 12:36 AM

mgahawa
Siku ya Jumatatu July 07 kwenye moja ya migahawa iliyopo eneo la Uzunguni Jijini Arusha,watu wanane waliripotiwa kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu.
Mkurugenzi wa makosa ya jinai wa Jeshi la Polisi Kamishna Issaya Mngulu amesema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa nane usiku ambapo watu wasiojulikana walirusha bomu hilo ndani ya mgahawa ujulikanao kamavama Traditional Indian Cusine uliopo jirani na viwanja vya Gymkhana jijini Arusha.
Pamoja na juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na Jeshi la Polisi za kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na yenye tulivu, bado kumeendelea kuwa na matukio ya kiuhalifu yakiwemo ya milipuko katika maeneo mbalimbali.
Kamishna Mngulu amenukuliwa akisema “Kufuatia kutokea kwa matukio haya bado tunaendelea na upelelezi wa kina ili kuhakikisha kwamba wale wote walioko kwenye mtandao huo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo  vya sheria”
Kamishna Mngulu anaendelea kwa kusema kuwa”Katika tukio hilo la jana tayari watu wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa uchunguzi zaidi lakini pia kati ya wale wanane waliojeruhiwa mmoja hali yake si nzuri hivyo amepelekwa Nairobi nchini Kenya kwa ajili ya matibabu zaidi”.
Aidha ameongeza kuwa, katika matukio mengine ya nyuma yaliyowahi kutokea mpaka sasa jumla ya watu 20 wamekamatwa wakiwemo sita wanaosadikiwa kujihusisha na mlipuko wa bomu uliotokea Julai 3 mwaka huu nyumbani kwa Shekhe Ally Sudi mkoani Arusha na wengine 12 katika tukio lililotokea mjini Zanzibar.
Hata hivyo Kamishina Mngulu ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kwa kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, vilevile wawe makini na mtu ama kitu watakachokitilia shaka ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.

0 comments:

Post a Comment