Wednesday, July 9, 2014

TUWE MAKINI: JINA LA MBUNGE HALIMA MDEE LATUMIKA KUWATAPELI WATU

By on 5:19 AM


MBUNGE wa Kawe jijini Dar es Salaam, Halima Mdee (CHADEMA) amewatahadharisha wananchi kuwaepuka watu wanaotumia jina lake katika mitandao ya kijamii wakidai wanatoa mikopo bila riba.
Alisema kuwa kadhia hiyo pia imewakuta baadhi ya wabunge wenzake wakiwemo wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) na wa Monduli Edward Lowassa (CCM).
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa simu, Mdee alisema kuwa ni wakati muafaka kwa Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi ili kuwabaini matapeli hao na kuwachukulia hatua kali za kisheria kwani wamechafua jina lake kwa kutapeli watu.
Alisema kuwa wamekuwa wakijitambulisha kama Mdee Community Loan na kutumia jina lake la Halima James Mdee wakidai kuwa ofisi zao zipo Mtaa wa Samora jengo la Jmall chumba no 490.
“Huu ni ujinga unaofanywa na hawa watu wenye lengo la kutuchafua, nawaomba wananchi kuwa makini na jambo hili na wanatumia namba ambazo ni 0753990581 au 0653918679.
“Ieleweke kwamba hakuna kitu kama hicho, sijawahi kutoa mikopo wala kuwa na kampuni inayojishughulisha na mambo hayo,” alisema Mdee.
Ameyaomba makampuni ya simu kuwa makini na kufanya uchunguzi ili kuweza kuwabaini matapeli hao kwani wao ni rahisi kuwafahamu kupitia mitambo yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alipoulizwa juu ya suala hilo, alisema hakuna kiongozi yeyote anayehusishwa na utapeli huo aliyetoa taarifa ya jina lake kutumiwa vibaya.
Alisema jeshi lake likipata taarifa hizo kwa usahihi litazifanyia kazi na kuwabaini wahusika wanaotumia majina ya watu wengine vibaya na kuwapotosha wananchi.
Tanzania Daima ilikutana na mmoja wa wahasibu katika jengo la Jmall (jina linahifadhiwa), na kusema katika jengo hilo, hakuna kampuni wala chumba chenye namba kama hizo zilizotajwa hapo juu.
“Katika jengo letu hatuna chumba namba 490 wala kampuni inayoitwa Community Loan, nawaomba Watanzania watambue kuwa hao ni matapeli,” alisema.
Chanzo:Tanzania Daima 

0 comments:

Post a Comment