Sunday, July 6, 2014

VIUNGO VYA BINADAMU VYATUPWA JALALANI MUHIMBILI, KUNGURU PAKA WAFANYA SHEREHE

By on 4:35 AM


Hospitali ya Taifa Muhimbili, inalazimika kutupa taka za hospitali jalalani vikiwamo viungo vya binadamu vilivyokatwa baada ya kukosekana kwa tanuru la kuchomea taka (insinereta) kwa zaidi ya miezi mitatu sasa. 
Kitendo hicho kinasababisha taka hizo kutoa harufu kali huku paka na kunguru wakichangamkia kufukua baadhi ya viungo hivyo vilivyotupa na kuvitawanya ovyo.

Baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo waliiambia NIPASHE kuwa tanuru hilo limeharibika zaidi ya miezi mitatu, huku kampuni ya K Environment iliyokuwa na zabuni ya kuzoa taka hizo, ikidaiwa kukatisha mkataba baada ya kutoelewana kwenye taratibu za malipo. Walidai kuwa hospitali imekuwa ikizikusanya taka hizo na kuzichoma nyakati za usiku.

Gazeti hili lilishuhudia mlundikano wa taka karibu na wodi ya wazazi ndani ya shimo lililokuwa  limechimbwa kwenye eneo lililo karibu na nyumba za wauguzi na madaktari.
Watumishi hao waliodokeza kuwa uchomaji wa taka hizo hufanywa usiku hivyo kujaza moshi na harufu karibu na nyumba zao.

Mmoja wa madaktari hospitali hapo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema: “uchomaji huo wa mabaki ya binadamu pamoja na sindano na dawa  sio salama.

 “Kitaalamu ili sindano iungue na kuyeyuka  huhitaji nyuzi joto zaidi ya 100 nashangaa uchomaji unaofanyika hapa.”

Alisema tanuru hilo lilianza kuleta usumbufu Juni mwaka jana ambapo ukarabati wake ulielezwa kuhitaji Sh. milioni 22.3.

“Hata baada ya kufahamu tatizo uongozi wa hospitali ulikuwa unafanya marekebisho madogo madogo ambayo gharama zilizotumika zinaweza kuzidi fedha ambazo zilitakiwa awali kwa ajili ya matengenezo.”

KUPUUZA TATIZO
Daktari huyo alibainisha kuwa tanuru lilipoanza kuwa na matatizo taka hizo zilikuwa zikipelekwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas)  kuchomwa na hospitali ilikuwa inatoa  fedha kugharamia kazi hiyo.

“Wakati taka zinazagaa jalalani, Mkurugenzi wa Muhimbili  amenunua gari la anasa aina ya Toyota Land Cruiser V8 ambalo thamani yake ni zaidi ya Sh. milioni 200,” kilisema chanzo kingine ndani ya ofisi ya kigogo huyo.

Aidha, chanzo hicho kimebainisha kuwa, ununuzi wa gari hilo umewashangaza wengi kwa kuwa fedha hizo zingeelekezwa kwenye kutatua kero mbalimbali zikiwamo vifaa ndani ya hospitali hiyo.

“Fedha za manunuzi ya gari hilo ambalo lina mwezi sasa zimepatikana wapi ikiwa zile za kutengeneza  insinereta  hazipo? Unanunua V8 wakati hospitali haina hela za kununua betri za mashine za kupima presha, huu siyo ubinadamu,” kililalamika chanzo chetu na kuongeza:

“Vifaa vya kupimia joto hizi ‘thermometer’ hakuna, utakuta  kwenye  wodi moja yenye wagonjwa 70 wanaohudumiwa na  wauguzi wawili  wananyang’anyana kipimajoto hiyo ndiyo hospitali kubwa ya rufaa ya taifa...” kimesema.

Baadhi ya wafanyakzi walihoji jukumu la kitengo cha ubora cha hospitalini hapo kuwa kazi yake ni nini kama hayo yote yanatendeka.

Baadhi ya wagonjwa waliofika hospitalini hapo walisema eneo la hospitali lipo kwa usalama wa afya za wanadamu hivyo uchafu huo ni chanzo cha  kuendeleza magonjwa ya  kuambukiza.

Walisema kuna chumba cha upasuaji na oparesheni zinafanyika kila wakati na uchafu uliorundikwa pale ni wa miili ya binadamu ambao unaliwa na paka na kunguru wanaoweza kubeba maradhi.

MAELEZO YA HOSPITALI
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Muhimbili,  Aminiel Aligaesha, alithibitisha kuharibika kwa tanuru hilo na kueleza kuwa taka hizo zilikuwa zikipelekwa Muhas kuteketezwa, lakini mashine ya chuo hicho nayo imeharibika na sasa zinachomewa jalalani.

Alibainisha kuwa taka hizo zinawekwa kwenye shimo la urefu wa mita mbili hadi tatu na dawa aina ya ‘povidone iodine’ inayoangamiza vimelea vya maradhi, vikiwemo virusi na fungasi inatumiwa. Pia wakati mwingine dizeli hutumiwa kuzichoma taka hizo.

Aligaesha alisema utaratibu huo hutumiwa kuzika wanyama waliokufa kwa maradhi ya kuambukiza kama kipindupindu na kimeta na kwamba hufanywa mbali na vyanzo vya maji.

“Mashine yetu iko kwenye matengenezo yanayotarajiwa kukamilika wiki ijayo,” alisema na kukanusha kuwa uchomaji unaofanyika huathiri afya za binadamu kwa vile utaalamu unatumiwa kuua vimelea vya maradhi.

UNUNUZI WA GARI
Aligaesha alikiri kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili amenunuliwa  gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 yenye thamani ya Sh. milioni 207 na kwamba limenunuliwa kwa sababu kwa miaka 10 mkurugenzi mtendaji hakuwahi kuwa na gari, badala yake alikuwa ameazimwa gari na Wizara ya Afya.

"Kabla ya kuazimwa gari hili mkurugenzi alikuwa akitumia pick up hata kwa safari za  nje ya hospitali,  ilifikia mahali hata ikitokea safari ya wakuu wa taasisi za afya kukutana nje ya Dar es Salaam, alikuwa akiomba lifti kwa wenzake," alisema na kutetea kuwa ununuzi wa V8  umefuata taratibu za kisheria.

MASHINE ZA BP
Aligaesha alisema  kuanzia mwezi Mei mwaka huu, wamepokea mashine 81 za kupimia presha ambazo kati ya hizo 75 zilitoka bohari ya dawa (MSD) na  sita zilikuwa za msaada.

Alibainisha kuwa mashine za  MSD zina uwezo mdogo wa kupima watu wengi lakini pia zinatumiwa kwa  muda mfupi na ili kuondoa tatizo hilo Muhimbili itanunua mashine nyingine zinazodumu zaidi kutoka nje ya MSD.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

0 comments:

Post a Comment