Sunday, July 6, 2014

WAZIRI MAGUFULI KUANZA ZIARA YA KIKAZI MIKOA YA MWANZA NA MARA

By on 4:42 AM


Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi katika mikoa ya Mwanza na Mara.

Katika ziara hiyo anatarajiwa kukagua na kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa kivuko kinachotarajiwa kufanya safari mithili ya daladala kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari jijini Mwanza.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo kwa vyombo vya habari, kivuko hicho cha Mv Temesa, kitazinduliwa Jumatano ijayo katika eneo ya Sweya, Nyegezi nje kidogo ya Jiji la Mwanza.

Kivuko hicho kilichofungwa mitambo ya kukiwezesha kusafiri kwa mwendo wa kasi ili kutoa huduma katika mwambao huo wa ziwa Victoria, kina uwezo wa kubeba tani 65 kwa wakati mmoja, sawa na abiria 80 na magari madogo matano. 

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kivuko hicho kitakuwa kinafanya kazi kutoka Luchelele kupitia Sweya, Butimba, Mkuyuni, Igogo hadi Kirumba, ikiwa ni mkakati wa kupunguza foleni katika jiji la Mwanza.

Serikali pia ina mpango wa kuanzisha kivuko cha aina hiyo, kitakachofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, lengo likiwa kupunguza msongamano.

Kabla ya uzinduzi wa kivuko hicho, Magufuli atakuwa na majukumu kadhaa ya kikazi kuanzia leo ambapo atakagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Usagara–Kisesa yenye urefu wa kilometa 16.7, inayojenga kwa kiwango cha lami.

Kesho, waziri huyo mmoja wachapakazi wanaopigiwa mfano katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, atakwenda mkoani Mara kukagua mradi wa barabara ya Makutano – Natta – Mugumu (sehemu ya Makutano – Sanzate) yenye urefu wa kilometa 50. 

Siku hiyo hiyo, atazindua rasmi kivuko cha Mv Mara kitakachotoa huduma kati ya Iramba na Majita. Baada ya uzinduzi huo, atafanya mkutano wa hadhara eneo la Mwibara ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa mradi wa Barabara ya  Nyamuswa–Bunda–Kisorya–Nansio (sehemu ya Bulamba–Kisorya) yenye urefu wa kilometa 51.

0 comments:

Post a Comment