VIJANA wanaotaka uongozi hususani nafasi ya urais, wameshauriwa kujenga
hoja, kuonesha malezi mazuri waliyo nayo na karama ya uongozi, ili watu
wabaini wawachague, badala ya kuegemea kigezo cha rika kuwapatia nafasi
husika.
Imeelezwa katika uchaguzi mkuu ujao, vyama vingi vinaweza kusimamisha
wagombea vijana kwa kuzingatia hoja inayotawala, ikageuka kete ya
kupandisha chama chati, lakini kwa upande wa kiongozi, akawa asiyefaa.
Wanasiasa kutoka vyama vya siasa tofauti, walisema hayo juzi kwenye
kipindi kilichokuwa kikirushwa moja kwa moja na televisheni ya Star
chini ya mada iliyosema, ‘Vijana na Kasi ya Kushika Madaraka; Je 2015 ni
wakati wao?’
Naibu Mkurugenzi, Mawasiliano wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya
alisema kama vigezo vya kupata kiongozi vikianza kuwa kutaka kuongozwa
na kijana, nchi inaweza kuongozwa na mtu asiyefaa.
Kambaya alitoa mfano wa Jaji Joseph Warioba, aliyetoa ushauri kwamba ni
vyema vijana washike hatamu, na kusema licha ya kwamba ni mzee,
alipopewa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, aliiongoza vizuri .
Kiongozi huyo wa CUF alisema, hekima, busara ya uongozi siyo tu
inatokana na maandalizi, bali pia na kipaji ambacho ni zawadi kutoka kwa
Mungu.
Alisisitiza kwamba matatizo ya Watanzania hayatokani na wazee, isipokuwa
ni ya kimfumo kwa maana kwamba hata kijana akiingia madarakani bila
mfumo kubadilika, yataendelea kuwepo.
“Uzee siyo ugonjwa na ujana si dawa ya matatizo tuliyokuwa nayo. Tatizo
ni la kimfumo. Hata aje kijana, mfumo tulio nao ndiyo utaendelea…ujana
hauwezi kuwa kete,” alisema Kambaya na kutolewa mfano wa baadhi ya
taasisi serikalini zinazoongozwa na zilizowahi kuongozwa na vijana
lakini zikafanya vibaya.
Kambaya alisema upo uwezekano mkubwa wa vyama vingi vya siasa,
kusimamisha mgombea kijana kwa kuzingatia hoja hiyo inayotawala na
inayojaribu kuaminisha jamii kwamba vijana ndiyo wanapaswa kupewa
nafasi.
Alisema, “inawezekana vyama vingi vikasimamisha vijana kwa kuzingatia
hoja inayotawla. Lakini hiyo itakuwa ni kupandisha vyama. Vitapata Rais
lakini anaelewa matatizo au ni tamaa ya kupata mali?.” Kiongozi huyo wa
chama aliendelea kusisitiza haja ya kutochagua rais kwa sababu ya ujana
wake.”Suala ni vigezo. Tukipiga chapuo ya vijana na wazee, hatutaondoa
matatizo yaliyopo.”
Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe na kada wa Chama Cha Mapinduzi,
Emmanuel Rutaraka, alisema ni vigumu kuwaengua wazee katika uongozi,
huku akisisitiza kiongozi ni lazima aandaliwe.
Akisisitiza dhana ya kuandaliwa, mwanasiasa huyo alitoa mfano wa Rais
Jakaya Kikwete na kusema alianza kuandaliwa tangu awali. Alisema wakati
Mwalimu Julius Nyerere akipigania uhuru, aliungwa mkono na wazee.
“Vijana wakubali kuandaliwa..ukisema wazee wakae kando, nani ataandaa
vijana,” alihoji Rutaraka aliyewahi kuwa Mbunge wa Bukoba Mjini
takribani miaka 30 iliyopita.
Mwanasiasa huyo mkongwe alikemea vijana wanaoponda wazee kwamba
wamepitwa na wakati, akisema, “hicho ni kiburi na ubinafsi kuwaambia
wazee wamepitwa na wakati.”
Alishauri vijana wanaotaka uongozi hususani nafasi ya urais, wajenge
hoja, waoneshe malezi mazuri na karama ili watu wakibaini hayo,
wawachague na siyo kutanguliza kigezo cha umri
0 comments:
Post a Comment