Saturday, July 5, 2014

JE UNAYAFAHAMU MASWALI 10 YA KUJIULIZA KABLA YA KUACHANA (TALAKA) : SOMA HAPA

By on 12:06 AM

Somo letu linahusu maswali ya kujiuliza kabla ya kuchukua uamuzi wa kuachana au kupeana talaka (kwa wanandoa). Binadamu si kama mbuzi, kwa maana hiyo wanapokutana, kunakuwa na sababu ya kukutana kwao, hivyo haitakiwi kuamua kuachana bila angalizo.
Wiki iliyopita nilikupa utangulizi unaojitosheleza kiufafanuzi, leo utaanza kujifunza au kujiongezea elimu kuhusu maswali 10 ambayo ama yanaweza kukufanya urudi nyuma na kuendelea kuujenga uhusiano wako au kushikilia msimamo wa kuachana lakini ukiwa na akili iliyo bora kabisa.

JE, UMEFANYA KILA LINALOWEZEKANA KUIOKOA NDOA/UHUSIANO WAKO?
Hapo kabla nimeshaeleza kwamba uhusiano wa kimapenzi hata kama haujakua na kuitwa uchumba au ndoa, nao una thamani yake. Binadamu si kama mbuzi kama wanaweza kuishi kama alivyoimba mwana-Bongo Fleva, Ali Kiba “Ukinipenda tunamalizana leoleo tu!”
Hapana! Uhusiano wa kimapenzi kwa binadamu lazima uwe na sababu ya kuanza, kwa hiyo na kufika mwisho inatakiwa kuwepo kwa hoja za msingi. Ni jambo lisilojaa akilini hata kidogo kwa watu wazima kuamua kuachana pasipo tafakuri ya aina yoyote.
Muongozo wa kitaalamu kwenye taaluma inayojenga uhusiano/ndoa imara na yenye afya, vilevile inayosherehesha kuachana katika taswira yenye nafuu ambayo haitakufanya uingie kwenye majuto ya baadaye, inakutaka ujiulize swali hili kabla ya kushabikia utengano.
Je, umefanya kila linalowezekana kuiokoa ndoa/uhusiano wako? Hapohapo ulipo, jiulize umeshafanya nini kuhakikisha unainusuru ndoa yako au umepambana kiasi gani kuulinda uhusiano wako usimezwe na mgogoro unaotamalaki kati yenu hivi sasa? Jawabu litakuongoza kuvuka salama.
Tambua kwamba katika uhusiano wowote ule wa kimapenzi lazima ukumbwe na misukosuko, kwa hiyo kuna nyakati utajikuta wewe na mwenzako mnapepesuka kiasi cha kuwafanya mkate tamaa ya kuendelea lakini mtakapokaa chini na kutafakari, mnaweza kujenga matumaini mapya.
Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton alikumbwa na mgogoro mkubwa kwenye ndoa yake kupitia kashfa ya mrembo Monica Lewinsky, aliyekuwa mtumishi wa Ikulu ya nchi hiyo, White House. Kama asingekaa na mkewe, Hillary Clinton kisha kujiuliza, leo hii wasingekuwa pamoja.
Clinton na Hillary baada ya kukaa pamoja na kutafakari umuhimu wa ndoa yao, waliziona nyakati zijazo ni zenye matumaini, furaha, amani na upendo, kwa hiyo wakachukulia mgogoro wa Lewinsky kuwa msukosuko kama wimbi linalokuja na kutoweka.
Zipo nyakati bahari huchafuka na kusababisha uhai wa msafiri na mvuvi kuwa shakani. Bahari hiyo baada ya machafuko hutulia na kuleta raha kwa mvuvi na msafiri. Chukulia uhusiano wako kama tabia za bahari, wewe na mwenzi wako hamtapepesuka mpaka mwisho, pengine nyakati zijazo zikawa ni zenye neema sana.
Tukirejea kwenye swali, kama ni kweli kwamba jibu lako ni “ndiyo”, kwamba umeshafanya kila linalowezekana kuuokoa uhusiano wako au ndoa yako na umeona hakuna matunda unayoweza kuvuna mbele ya safari, basi usikilize moyo wako.
Hillary aliamini kuwa pamoja na usaliti wa mumewe kwa Lewinsky, lakini Clinton ni mali yake, cha kufanya ni kumsahihisha ili makosa yaliyojitokeza yasijirudie tena. Kweli, baada ya msukosuko huo, maisha yao yamekuwa yenye raha na ushirikiano mkubwa.
Kwa kitendo cha Hillary kujenga matumaini kwa mumewe, Clinton alimsaidia kushinda ndoto zake za kuwa Seneta wa Jimbo la New York na baadaye kugombea hatua za awali urais wa Marekani kabla ya kushindwa kwenye chama chake cha Democrat na Rais Barack Obama ambaye alimteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Hata Obama na Michelle wamekuwa wakiingia kwenye misuguano ya hapa na pale lakini kitu kikubwa ni kuvumiliana na kuamini kwamba zipo nyakati bora zaidi baadaye. Wanafanya kila linalowezekana kuufanya uhusiano wao uendelee kuwa hai.
Ni ukweli kuwa jitihada za kuuokoa uhusiano zinapaswa kufanywa na pande zote mbili. Haiwezekani mmoja awe anaota matarajio chanya mwingine hayaoni. Jitahidi kumfanya mwenzi wako ayaone maisha bora ya baadaye, ikishindika basi utakuwa umefanya kila linalowezekana bila mafanikio.
Kama hujafanya linalowezekana basi fanya kuanzi sasa.
Siku zote katika maisha yako, uamuzi wa kuachana na mwenzi wako, unapaswa kuwa wa mwisho, yaani baada ya kujiridhisha kwamba kila jitihada umefanya lakini hazikuzaa matunda. Kwa hatua hiyo, hutajuta baadaye!
SOURCE:GP
<<KWA HABARI ZAIDI BOFYA HAPA ULIKE PAGE HAPA>> 

0 comments:

Post a Comment