Dar es Salaam. Waziri Mkuu
mstaafu, Jaji Joseph Warioba ametoa dira ya urais katika Uchaguzi Mkuu
ujao kwa kutaja sifa za rais anayefaa kuiongoza Tanzania.
Warioba alisema kwamba taifa la Tanzania
linastahili kuongozwa na vijana wenye nguvu ya mwili na akili. “Mimi
nafikiri tuangalie kati ya vijana tulionao, nani anatufaa kuiongoza
nchi, tusirudi kuangalia wazee,” alisema Jaji Warioba.
Alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali ya
mwandishi wa habari hizi katika mahojiano maalumu yaliyofanyika wiki hii
ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo ya Jaji Warioba imekuja huku ukiwa
umesalia takribani mwaka mmoja na miezi minne, kabla ya taifa kuingia
kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani
utakaoshirikisha vyama zaidi ya 23 vyenye usajili wa kudumu nchini.
Uchaguzi huo mkuu ambao ni wa tano wa vyama vingi
nchini, unatarajiwa kulipatia taifa rais mpya, baada ya Rais Jakaya
Kikwete kumaliza muda wake wa utawala wa awamu ya nne.
Mbali na wagombea wa vyama vya upinzani, ndani ya
CCM pekee kunatajwa kuwa na makundi zaidi ya manne yanayotarajia kuwania
urais mwaka ujao.
Makundi hayo ni pamoja na linalotajwa kumuunga
mkono Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, kundi lingine linatajwa kuwa
nyuma ya Samuel Sitta ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki pamoja na linalomuunga mkono Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Sera
na Uratibu, Stephen Wassira anatajwa kuwania nafasi hiyo ya juu ya
uongozi nchini.
Hata hivyo, viongozi hao wamekuwapo madarakani
katika nyadhifa na nyakati tofauti huku pia wakiwa na umri uliovuka
ujana, unaopendekezwa na Jaji Warioba.
Ndani ya CCM vijana wanaotajwa kutaka kuwania
urais mwakani ni pamoja na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini,
William Ngeleja na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January
Makamba.
Makamba tayari ametangaza nia yake ya kuwania
urais akisema huu ni wakati wa kupisha fikra mpya kuongoza dola, licha
ya chama hicho kuzuia kutangaza nia na kupiga kampeni kabla ya muda.
Makamba, mmoja wa makada wa CCM walioonywa na
chama hicho baada ya kutuhumiwa kuanza kampeni mapema, alijipigia debe
kuwa iwapo atapitishwa na chama hicho, ataelekeza nguvu kwenye
vipaumbele vinne ambavyo ni ajira, huduma za jamii, uchumi imara na
utawala bora. Akizungumzia uzoefu Makamba alisema hakuna ushahidi wowote
kwamba miaka mingi kwenye siasa ndiyo inatengeneza kiongozi mzuri.
“Uongozi mzuri unatengenezwa na haiba, wajihi,
dhamira, uwezo, maadili, uhodari, hekima na maarifa. Sifa hizi
hazipatikani kutokana na uzoefu wa miaka mingi kwenye siasa hata baadhi
ya vijana wanazo,” alisema Makamba.
SOURCE:MWANANCHI
<<KWA HABARI ZAIDI BOFYA HAPA ULIKE PAGE HAPA>>
<<KWA HABARI ZAIDI BOFYA HAPA ULIKE PAGE HAPA>>
0 comments:
Post a Comment