MBUNGE wa Kawe jijini Dar es Salaam, Halima Mdee (CHADEMA)
amewatahadharisha wananchi kuwaepuka watu wanaotumia jina lake katika
mitandao ya kijamii wakidai wanatoa mikopo bila riba.
Alisema kuwa kadhia hiyo pia imewakuta baadhi ya wabunge wenzake
wakiwemo wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) na wa Monduli
Edward Lowassa (CCM).
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa simu, Mdee alisema kuwa ni
wakati muafaka kwa Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi ili kuwabaini
matapeli hao na kuwachukulia hatua kali za kisheria kwani wamechafua
jina lake kwa kutapeli watu.
Alisema kuwa wamekuwa wakijitambulisha kama Mdee Community Loan na
kutumia jina lake la Halima James Mdee wakidai kuwa ofisi zao zipo Mtaa
wa Samora jengo la Jmall chumba no 490.
“Huu ni ujinga unaofanywa na hawa watu wenye lengo la kutuchafua,
nawaomba wananchi kuwa makini na jambo hili na wanatumia namba ambazo
ni 0753990581 au 0653918679.
“Ieleweke kwamba hakuna kitu kama hicho, sijawahi kutoa mikopo wala
kuwa na kampuni inayojishughulisha na mambo hayo,” alisema Mdee.
Ameyaomba makampuni ya simu kuwa makini na kufanya uchunguzi ili
kuweza kuwabaini matapeli hao kwani wao ni rahisi kuwafahamu kupitia
mitambo yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alipoulizwa
juu ya suala hilo, alisema hakuna kiongozi yeyote anayehusishwa na
utapeli huo aliyetoa taarifa ya jina lake kutumiwa vibaya.
Alisema jeshi lake likipata taarifa hizo kwa usahihi litazifanyia
kazi na kuwabaini wahusika wanaotumia majina ya watu wengine vibaya na
kuwapotosha wananchi.
Tanzania Daima ilikutana na mmoja wa wahasibu katika jengo la Jmall
(jina linahifadhiwa), na kusema katika jengo hilo, hakuna kampuni wala
chumba chenye namba kama hizo zilizotajwa hapo juu.
“Katika jengo letu hatuna chumba namba 490 wala kampuni inayoitwa
Community Loan, nawaomba Watanzania watambue kuwa hao ni matapeli,”
alisema.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment