Sunday, July 6, 2014

SINGIDA YAKABILIWA NA UPUNGUFU WA WATUMISHI SEKTA YA AFYA

By on 4:40 AM


Na Nathaniel Limu
HALMASHAURI ya wilaya ya Singida, inakabiliwa na upungufu wa watumishi 144 wa kada mbali mbali wa sekta ya afya, hali inayosababisha huduma za afya kutolewa bila kuzingatia ubora unaohitajika
Hayo yalisemwa na Katibu wa afya katika halmashauri hiyo,Severin Sosthenes, wakati akitoa majibu dhidi ya hoja zilizotolewa na timu ya ufuatiliaji uwajibikaji jamii (Social Accountability Monitoring – SAM) katika halmashauri hiyo.
Alisema halmashauri hiyo ina mikakati kadhaa ya kutatua tatizo la upungufu wa raslimali watu katika sekta ya afya.
Katika mikakati hiyo, alisema katika bajeti yao ya mwaka juzi, walitenga fedha kwa ajii ya watumishi wapya 110.
“Baada ya kutenga fedha hizo, tulizunguka vyuo mbali mbali kuhamasisha wanaomaliza masomo, waombe kuja kufanya kazi kwenye halmashauri yetu,na tukawahakikishia kuwalipa stahiki na stahili zao”,alifafanua katibu huyo.
Sosthens alisema pamoja na juhudi hizo, walifanikiwa kupata watumishi 47 wa kada mbali mbali ambao hadi sasa wanaendelea kufanya kazi katika halmashauri hiyo ingawa idadi inayohitajika bado haijafikiwa.
Katika hoja yake hiyo, timu ya SAM ilitaka kujua ni jinsi gani halmashauri imejipanga kuhakikisha inatatua tatizo la raslimali watu katika sekta ya afya.
Pia ilitaka kujua halmashauri hiyo ina mpango gani mahususi uliopo kwa ajii ya kuhakikisha watumishi hawakimbii vituo vyao vya kazi.
Timu ya SAM imebaini mapungufu mbali mbali katika zahanati na vituo vya afya ktika halmashauri hiyo, ikiwemo baadhi ya paa za baadhi ya zahanati na vituo vya afya kuwa na makazi ya nyuki, kila kinachohatarisha usalama wa wagonjwa.
Mapungufu mengine ni uchakavu wa majengo, pikipiki za magurudumu matatu ambazo zilikuwa zitumike kuwabeba wagonjwa kushindwa kufanya kazi katika mazingira ya vijijini na uhaba wa masanduku ya maana na mbao za matangazo.
Hata hivyo timu ya SAM, imeipongeza halmashauri hiyo, kwa kupata hati safi ya mkaguzi wa mahesabu ya serikali kwa miaka mitatu mfululizo.
Pia halmashauri hiyo imepongezwa pamoja na idara ya afya kuwezesha upatikanaji wa madawa muda wote katika vituo vya kutolea huduma ya afya, na kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya.

0 comments:

Post a Comment