Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Askari Magereza
wa kike aliyejeruhiwa kwa risasi baada ya basi la jeshi hilo
kushambuliwa kwa risasi na majambazi, amesema hakuhisi mpenyo wa risasi
katika titi lake la kushoto mpaka alipokaguliwa na askari mwenzake.
Askari huyo ni
mmoja wa majeruhi ambao walishambuliwa kwa risasi kwenye basi la Jeshi
la Magereza lililokuwa limebeba mahabusu, Julai 2, mwaka huu, baada ya
kupora fedha kwenye gari lingine lililokuwa kwenye foleni, eneo la
Msasani kwa Mwalimu Nyerere karibu na Hoteli ya Regency.
Akizungumza na
gazeti hili jana kwa taabu, Koplo Doto Sanga aliyelazwa Hospitali ya
Taifa Muhimbili wodi namba 12 Kibasila, anasema ilichukua muda kuhisi
maumivu ya risasi hiyo, kwani iliambatana na vioo wakati majambazi hao
wanne waliposhambulia kioo cha mbele cha basi hilo.
“Ninachokumbuka
siku hiyo tulikuwa tumetoka Kawe tunaelekea mahakama ya Kinondoni nikiwa
na mahabusu wa kike, saa 8:30 mchana baada ya kufika maeneo ya
Mikocheni tulikutana na foleni kwa kuwa tulikuwa tunawahisha mahabusu,
dereva ‘alitanua’ (kupita pembezoni mwa barabara kukwepa foleni),”
anasema Koplo Sanga na kuongeza:
“Ghafla tukaona
uporaji ukifanyika mbele ambako tulikuwa tunaelekea, baada ya majambazi
wale kutuona wakaona sisi tayari ni kikwazo kwao hapohapo nikawasihi
mahabusu wote walale chini, wakatokea watu wawili na kushambulia basi
tulilopanda kwa risasi mbele na nyuma, baada ya kuanza kwa zoezi hilo
mimi, dereva na askari mwingine tukalala chini pia,” anasema.
Koplo huyo
aliyelitumikia jeshi la magereza kwa miaka 14 sasa, anasema risasi
ziliendelea kurindima kwa dakika chache na baadaye majambazi hao
walikimbia.
“Haikuchukua muda
mrefu, majambazi wale walikimbia, baada ya kunyanyuka tuliamua kuanza
kukaguana kwanza, tuliona dereva alikuwa amejeruhiwa mkononi na kuna
mahabusu wa kike naye alijeruhiwa kichwani lakini hakuna risasi
iliyopenya mwilini.
“Wakati
tukiendelea kukaguana mahabusu mmoja akaniuliza iwapo kifuani mwangu
nimechomwa na kitu, nilipoangalia ndipo nikagundua kwamba kuna kitu
kimeingia ndani na baadaye nikajua ni risasi, na hapo ndipo nikaanza
kuhisi maumivu,” anasema Sanga aliyejiunga na jeshi hilo mwaka 2000.
Anasema ghafla
akaanza kukohoa damu na hapo ndipo walipoamua kumwahisha katika
Hospitali ya TMJ ili kupatiwa huduma ya kwanza, kabla ya kumwamishia
Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Alisema dhumuni
la majambazi hao wanne lilikuwa ni kupora fedha kutoka kwa mtu mmoja
aliyekuwa ametokea ATM kuchukua kiasi cha Sh1 milioni.
0 comments:
Post a Comment