KWA UFUPI
- Dawa zinazotumika kuchora tattoo nyingi zina sumu na mashine zinazotumika husambaza maambukizi ya magonjwa.
Siku hizi hapa nchini ni jambo la kawaida kuona watu hasa vijana wakiwa wamejiremba miili yao kwa michoro, maarufu kama tattoo.
Michoro hii huwa inalenga sababu na maana mbalimbali, ingawa jambo hili kwa vijana huonekana kama kwenda na wakati. Wakati mwingine michoro hiyo huandamana na imani za kishirikina katika kutekeleza malengo fulani.
Mara nyingi alama hizi zinaweza kuwa ni michoro ya maua, picha za watu au wanyama, ramani na hata wakati mwingine inaweza ikawa haieleweki.
Alama au michoro zisizoeleweka huchorwa maeneo ya wazi au yaliyojificha ambayo huonekana pale tu mtu akiwa amevua nguo.
Alama kwenye maeneo ambayo huweza kufichwa ni kama vile misuli ya mikono, mabega, kifua, tumbo, mgongo, mapaja, makalio na maeneo yanayozunguka sehemu za siri. Maeneo ya wazi ni paji la uso, mikono, vidole, visigino au miguuni.
Michoro hii huweza kuchorwa kwa ajili ya kipindi fulani tu au ya kudumu kulingana na malengo na kusudio la mhusika.
Yale ya muda huweza kuchorwa kwa ajili ya tukio kama vile michezo, kuolewa ama sherehe mbalimbali ambazo huhusisha wanawake.
Kuna wanaotumia rangi zinazotokana na mimea ya kawaida na wengine hutumia dawa maalumu zinazouzwa madukani pamoja na vifaa vya kuchorea.
Wanasayansi wa afya ya jamii wanaonya kuwa michoro iliyotokana na rangi za madukani pamoja na vichoreo vyake, inaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa wahusika.
Baadhi ya rangi zinazotumika kuchora mapambo mwilini zinaweza kusababisha mzio wa ngozi katika eneo la mwili mahali palipo na tattoo. Mzio huu unaweza kutokea kipindi kirefu baada ya kuchora tattoo.
Tafiti nyingi za kitabibu pia zinaonesha kwamba, wino au rangi za tattoo zinaweza kusababisha uambukizo wa bakteria aina ya mycobacterium cholonae.
Bakteria hawa wanaweza kusababisha magonjwa ya ngozi na nyama za mwili, matatizo ya njia ya mkojo, tatizo kwenye mfumo wa kupumua, magonjwa ya uambukizo kwenye mifupa, uambukizo katika nyama za moyo, homa ya uti wa mgongo na tatizo la macho.
SOURECE:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment