Friday, July 4, 2014

Ana kwa ana na Edward Lowassa... KVP SOMA ZAIDI HAPO

By on 3:16 AM


Waziri Mkuu wa zamani na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza wakati wa mahojiano na waandishi wa gazeti hili mjini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi 

KWA UFUPI
  • Yafuatayo ni mahojiano ya Mwananchi na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa. Hata hivyo Lowassa hakuwa tayari kuzungumzia masuala yanayohusu uchaguzi mkuu ujayo na mambo yanayohusiana na hilo kwa sababu anatumikia adhabu ya kusimamishwa mwaka moja na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Yafuatayo ni mahojiano ya Mwananchi na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa. Hata hivyo Lowassa hakuwa tayari kuzungumzia masuala yanayohusu uchaguzi mkuu ujayo na mambo yanayohusiana na hilo kwa sababu anatumikia adhabu ya kusimamishwa mwaka moja na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Swali: Umekuwa ukisema mara kwa mara kuwa tatizo la ajira ni bomu linalosubiri kupasuka, je serikali ifanye nini kukabiliana na tatizo hilo?
Lowassa: Duniani kote vyama vya siasa vinapotaka kuingia madarakani huangalia masilahi ya watu, huangalia ni jambo gani la msingi ambalo chama kikiingia madarakani kitayafanya. Suala la ajira lipo karibu katika kila nchi, kila chama kinachoingia madarakani hulizungumza hilo.
Labda niseme mfano mmoja, Mwalimu (Julius) Nyerere alipokuwa anaanzisha elimu ya kujitegemea mwaka 1967 alikuwa anaangalia ajira. Aliangalia akaona hatuna viwanda, kwa hiyo elimu ikawa lazima iwe ya kujitegemea. Unamuandaa mwanafunzi kwa maisha ambayo yatamuajiri vijijini. Mwaka 1967, Mwalimu Nyerere alikuja na elimu ya kujitegemea, kwa hiyo ni lazima na sisi tuje na mawazo mapya ya ajira. Kwanza hakuna ubishi kwamba watu wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha sita, vyuo, vyuo vikuu na kadhalika ni wengi sana. Watu wote hawa wanaangalia kwamba wanafanyiwa nini katika ajira.
Kwa hiyo mimi sisemi tu ni bomu, ila nasema ni bomu linalotarajia kulipuka wakati wowote. Lakini ni bomu ambalo tunahitaji kulishughulikia. Lengo langu la kupiga kelele ni kuitaka jamii ishughulikie jambo hili. Nashukuru nilipopiga kelele kidogo, wizara zilitoa takwimu na kila wizara ikatakiwa kuangalia kwenye eneo lake inatengeneza ajira kiasi gani, mimi nasema huo ndiyo mchakato.
Lakini kwa maoni yangu, ajira ya Tanzania lazima iangalie kwenye eneo kubwa la kilimo. Kilimo ndicho kinachochukua ajira ya watu wengi nchini. Lakini sasa tukiwapeleka vijana kwenye kilimo tutengeneze mazingira ya kumfanya mwanafunzi anayemaliza chuo kikuu awe tayari kuishi mazingira ya kilimo.
Nilipokuwa Waziri wa Maji nilitembelea Misri, kule mwanafunzi anapomaliza chuo kikuu anapelekwa Mto Nile anapewa ekari tatu za kulima mizabibu, anapewa trekta na vyombo vingine na anapewa mkopo ambao ataanza kuulipa baada ya miaka mitatu.
Pia tangu akiwa chuo, anajua ajira yake ni kilimo na kwamba atapewa mazingira ya kufanya kilimo; si cha jembe la mkono ila kilimo cha kisasa. Anakopeshwa na anawezeshwa. Kwa hiyo mimi nasema jambo moja kubwa sana la kufanya ni kuhakikisha tunawapeleka vijana kwenye kilimo, lakini kilimo chenye mabadiliko. Kilimo ambacho ni cha kisasa zaidi ambacho atakifurahia na ambacho kitamletea maisha bora katika maisha yake.
Eneo jingine mimi nadhani tungefanya uamuzi magumu ni kutenga maeneo tukapanda michikikichi (mawese), kama ilivyo Kigoma.
Tuchukue ekari kama milioni 10 tupande michikikichi, michikichi hii tuigawe. Kwa mfano tungeweza kufanya kazi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), iwe ni kuhakikisha wanaanzisha mashamba ya michikichi. Mkishaanzisha mashamba ya michikichi, mnawakabidhi vijana ambao hawana ajira waendelee na michikichi na baada ya miaka mitatu au minne watakuwa wamevuna, hali yao itakuwa nzuri na utakuwa na mafuta ya chakula nchini, tutakuwa na mafuta ya ku-export (kuuza nje) na utakuwa umetengeneza ajira kwa vijana wengi.
Vilevile la tatu ni eneo kubwa ambalo linategemewa na watu; ni viwanda. Na mtakumbuka wakati (Rais wa Marekani, Barack) Obama anagombea urais kwa mara ya pili wale wafanyakazi wa General Motors (kiwanda kikubwa cha magari Marekani) waliandika bango ‘You saved our jobs in September, this year we will save your job in November (Uliokoa ajira yetu Septemba nasi tutaokoa  ajira yako Novemba) wakimkumbuka alivyofanya uamuzi ambao si wa kibepari; ulikuwa ni wa kijamaa, kwamba serikali inawekeza kwenye viwanda.
Kwa siasa za kibepari jambo hilo halipo, lakini serikali ililazimika kuwekeza kwenye viwanda ili ajira ziendelee na viwanda viendelee. Sasa mimi nasema tunaweza na sisi tukajenga viwanda makusudi vya nguo ambavyo vinachukua ajira ya watu wengi au viwanda vingine tutakavyoona vinafaa vinavyochukua ajira ya watu wengi.
<<KWA HABARI KILA SIKU BOFYA HAPA NA LIKE PAGE HAPA>>

0 comments:

Post a Comment