Vijana wawili waliokuwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chemchem wilayani Mkalama katika Mkoa wa Singida, wamehukumiwa kifungo cha miaka sita kila mmoja baada ya Mahakama kuwatia hatiani kwa kosa la mauaji ya mwalimu wao.
Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma inayoendesha vikao vyake mjini Singida, ilitoa hukumu hiyo jana.
Waliohukumiwa
ni Shani Mtua na Mohammed Salimu ambao wakati walipotenda kosa hilo,
mwaka 2008, walikuwa Kidato cha Tatu na walikuwa na umri wa miaka 18
kila mmoja.
Ilielezwa
mahakamani kwamba kulikuwa na washitakiwa wengine wawili katika kesi
hiyo; Emmanuel Daud na Michael Msengi, walikufa wakiwa mahabusu
wakisubiri kesi yao kusikilizwa na Mahakama Kuu.
Hukumu
ilitolewa na Jaji Rehema Mkuye baada ya washitakiwa hao kukiri shitaka
la kuua bila kukusudia walilofanya katika Kijiji cha Mpambala, Tarafa
ya Kirumi Wilaya ya Mkalama.
Awali,
Mwanasheria wa Serikali, Zakaria Elisaria aliyekuwa anasaidiwa na
Karen Mrango, alidai mahakamani kwamba washitakiwa walihusika na mauaji
ya Rajabu Idude (49), aliyekuwa Mwalimu wa Nidhamu shuleni hapo.
Ilidaiwa walifanya mauaji hayo Agosti 2008.
Mwanasheria
huyo wa Serikali alidai chanzo cha mauaji hayo ni mshitakiwa wa kwanza ,
Shani, kupewa barua ya kusimamishwa masomo kwa wiki mbili kutokana na
utovu wa nidhamu na kisha akashawishi wenzake watatu kumpiga mwalimu
huyo.
Zakaria
alisema wanafunzi hao walimvizia mwalimu huyo katika kichaka cha karibu
na shule yao wakampiga ngumi na mateke, kisha wakamjeruhi mwilini kwa
kisu alichokuwa nacho mshitakiwa wa kwanza.
Inadaiwa
kutokana na kipigo hicho, Mwalimu Idude alipiga kelele na mwanawe
aliyetajwa kwa jina la Maye Rajabu, alifika haraka kwenye eneo la
tukio, lakini akakuta ameshakufa.
Wanafunzi
hao (washitakiwa) hawakukutwa katika eneo hilo lakini msako ulifanyika
usiku huo na wanafunzi wanne walikamatwa. Baada ya kuhojiwa kuanzia
ngazi ya mlinzi wa amani kwenye kijiji hicho hadi jana mahakamani,
walikiri kosa.
Kwa
upande wake, Wakili wa washitakiwa, kutoka Kampuni ya Uwakili ya Kim
& Company, Raymond Kimu, alimwomba Jaji Mkuye kutoa adhabu nafuu
dhidi ya wateja wake, kutokana na kuonesha ushirikiano wa kutosha tangu
siku waliyokamatwa.
Aidha,
alidai washitakiwa walifanya kosa hilo kutokana na kusukumwa na umri
mdogo wa utoto. Alidai ni wakosaji wa mara ya kwanza, wanajutia kosa
hilo na kwamba wamekaa jela kwa muda mrefu wa miaka sita, hivyo
wamejifunza kutokana na mauaji hayo.
Akitoa
hukumu, Jaji Mkuye alisema hakuna ubishi kwa yote aliyosema wakili wa
utetezi. Hata hivyo alisema, anadhani sababu hizo siyo kibali kwa
washitakiwa hao kupanga na kutekeleza mauaji dhidi ya mwalimu wao
aliyekuwa anasimamia nidhamu.
“Nadhani
kosa walilofanya haliwezi kukubalika kwa jamii hata kidogo…fujo
zimekuwa zikitokea kwenye mashule na vyuo, hata kusababisha vurugu kiasi
cha kuathiri utendaji…, kufuatia kosa hili, kila mmoja atatumikia
kifungo cha miaka sita jela,” alisema Jaji Mkuye.
0 comments:
Post a Comment