WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ametembelea Maonesho ya 38 ya Kimataifa ya
Biashara na kueleza kutoridhishwa na ubora na mvuto wa eneo la maonesho.
Amesema umefika wakati eneo hilo, Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere
vilivyopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, linapaswa kubomolewa
na kujengwa upya na kisasa.
Pinda alisema pamoja na kuongezeka kwa mataifa makubwa kushiriki katika
maonesho hayo, lakini eneo la maonesho halina mvuto wa kimataifa.
Alisema ni vema kusimamisha maonesho hayo hata kwa mwaka mmoja ili
kuvunja majengo yote na kujenga upya kwa kutumia taasisi za ndani kama
Benki ya Uwekezaji (TIB) au Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)
kwani kwa fedha za ndani inawezekana kuleta mvuto.
“Lazima kufanya uamuzi sasa wa kubomoa uwanja huu na kujenga upya hata
ikibidi kusimama maonesho kwa mwaka mmoja na kujenga kwani hata njia za
kupita ni finyu za tokea zamani lazima kubadilishana kuwa na wakati kama
maonesho yalivyo,” alisema Pinda katika ziara yake ya saa mbili,
alitembelea mabanda mbalimbali yakiwemo, Banda la Asali, Banda la
Kampuni ya Property International, TIB, Mamlaka ya Elimu ya Ufundi
Tanzania (VETA) na Banda la Tanzania.
Katika hatua nyingine, alisema sekta binafsi ina uwezo wa kufanya mambo mazuri katika kukuza uchumi.
Alitoa mfano wa Chuo cha Global Link Education kinachounganisha
wanafunzi kusoma nje ya nchi, zaidi kwenye vyuo vinavyotambulika, hivyo
kuondoa changamoto ya vijana kurudi na vyeti vya nje ya nchi visivyo na
ubora.
Pinda alisema chuo hicho kimesaidia kuondoa urasimu uliopo serikalini
katika kushughulikia ufadhili nje ya nchi kwa kutoza gharama ndogo, huku
wakieleza kwa uwazi nafasi na nchi zenye vyuo vizuri vya taaluma
mbalimbali.
Waziri Mkuu alieleza pia kufurahishwa na benki za NMB na TIB kusaidia
wajasiriamali wadogo. Kwa mujibu wake, NMB pekee imesaidia Sh bilioni 50
jambo ambalo ni mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi.
Aliomba benki zote nchini kungalia namna ya kukuza mradi huo wa kusaidia
wafanyabiashara wadogo nchi nzima ikiwemo ukopeshaji wa baiskeli za
miguu mitatu yaani bajaj na pikipiki huku wakiwapatia mafunzo kwanza
kuepuka ajali.
0 comments:
Post a Comment