JESHI
la Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia watu
nane wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi sugu. Wawili kati yao wanahusishwa
na tukio la kuuawa kwa Sista Cresencia Kapuri (50) wa Kanisa Katoliki
Jimbo Kuu la Dar es Salaam katika Parokia ya Makoka.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jana.
Alisema wahutuhumiwa hao, wakiwa katika utekelezaji wa uhalifu wao, walisababisha vifo, majeraha, wizi wa mali na fedha taslimu.
Alisema
watuhumiwa hao, walitumia silaha za moto, ikiwa ni pamoja na bunduki
aina ya SMG, bastola na vifaa mbalimbali vya uvunjaji, ikiwa ni pamoja
na baruti.
Alitaja
watuhumiwa wanaohusishwa na tukio la kuuawa kwa Sista Cresencia kuwa ni
Manase Ogenyeka (35), maarufu kama Mjeshi, mkazi wa Tabata Chang’ombe
Manispaa ya Ilala, ambaye ni dereva wa bodaboda ; na Hamisi Shaaban
maarufu kama Carlos, mfanyabiashara, mkazi wa Magomeni Mwembechai
Manispaa ya Kinondoni.
Sista
huyo aliyekuwa pia Mhasibu wa Parokia ya Makoka na Mhasibu wa Shule ya
Mwenyeheri Anwarite inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, aliuawa kwa
kupigwa risasi Juni 23, mwaka huu katika eneo la Riverside, Ubungo
Kibangu, Dar es Salaam. Kova alisema licha ya kuhusishwa na kifo cha
Sista huyo, watu hao wanatuhumiwa kupora Sh milioni 20.
Alisema
watuhumiwa hao, pia walikuwa wakitafutwa kwa muda mrefu kwa tuhuma za
uporaji wa Benki ya Barclays Tawi la Kinondoni, uliotokea Aprili 28,
mwaka huu, ambapo mamilioni ya fedha yaliibwa kabla na baada ya tukio
hilo.
“Jambazi
Manase Ogenyeka ndiye aliyeendesha pikipiki, akimbeba mwenzake akiwa na
fuko la mamilioni ya fedha na kutoroka nazo wakati Hamisi Shaaban ndiye
aliyekuwa kiongozi katika tukio hilo,” alidai Kova.
Mbali
ya kuuawa kwa Sista Cresencia, katika tukio hilo aliongozana na Sista
Brigita Mbaga (32) na dereva wao, Mark Mwarabu, aliyekuwa akiendesha
gari aina ya Toyota Hilux Pick-Up, lenye namba T213 CJZ ambaye alikatwa
dole gumba lake kwa risasi baada ya kushambuliwa.
Alisema
Jeshi la Polisi, bado linawatafuta watuhumiwa wengine wawili katika
tukio la kuuawa kwa Sista. Mtu mwingine anayetafutwa ni Leonard Molel
anayetuhimwa kwa tukio la wizi katika Benki ya Barclays.
Kamanda
huyo alisema watuhumiwa wengine watatu, kati ya hao wanane, walikamatwa
baada ya kutumia mbinu ya hati bandia wakiwa wanaomba kazi katika
kampuni binafsi ya ulinzi iitwayo Instant Security Services Mtaa wa
Makangira Msasani, Dar es Salaam.
Hao ni Elibariki Makumba (30) na Nurdin Suleimani (40), wakazi wa Buguruni Madenge na Mrumi Salehe(38), mkazi wa Kigogo Fresh.
Alitoa
rai kwa kampuni za ulinzi, yanapotaka kuajiri walishirikishe Jeshi la
Polisi ili wafanye upekuzi wa pamoja, utakaohusisha alama za vidole,
picha na ukaguzi wa kumbukumbu muhimu za kibayolojia kama vile vipimo
vya DNA.
Aidha,
aliwaomba wananchi ambao wana tabia ya kutembea na fedha nyingi, kuacha
kufanya hivyo, kwani kwa sasa teknolojia imepanuka, hivyo kuweza
kutumia simu za mkononi kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda
nyingine.
Credit: Habari leo
Credit: Habari leo
0 comments:
Post a Comment